Naibu rais Ruto akiri kuwa kiongozi wa upinzani, ashtumu upinzani kwa kutelekeza wakenya

Muhtasari

• Ruto alisisitiza kuwa kimya kutoka kwa wizara husika huku hali ikizidi kuwa mbaya ni jambo la kutia wasiwasi.

• "Jukumu tunalotekeleza hapa ni kwa sababu tunaamini katika uraia wa jamhuri yetu," Ruto alisema.

• Alisema Wakenya sasa wanasubiri hatua kutoka kwa wizara ya Hazina ya Kitaifa, Kilimo na Petroli.

Naibu Rais William Ruto siku ya Jumatatu alieleza ni kwa nini amelazimika kutekeleza majukumu ya upinzani.

Kulingana na Ruto, ni jukumu linalofaa kutekelezwa na mtu mwingine, lakini hana budi kulitekeleza kwa sababu ana masilahi ya Kenya moyoni.

"Hili ni jukumu la mtu mwingine lakini tunalazimika kufanya hivyo kwa sababu tuna masilahi ya taifa moyoni na tunataka kulainisha mambo nchini Kenya.

 Tungeamua kunyamaza, lakini mgogoro unaoshuhudiwa nchini Kenya hauwezi kuturuhusu kukaa kimya," alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika makazi yake ya Karen.

"Jukumu tunalotekeleza hapa ni kwa sababu tunaamini katika uraia wa jamhuri yetu."

Naibu rais ambaye ni wa pili katika mamlaka serikalini alishutumu upinzani kwa kuacha wajibu wao kwa sababu ya ulafi, na kujiunga na serikali na sasa wamegeuka kuwa wafisadi wakuu.

Alisisitiza kuwa hali hii imefanya iwe vigumu kwa wananchi kuiwajibisha serikali.

"Unajua iliyokuwa serikali sasa imegeuka kuwa upinzani na uliokuwa upinzani sasa umejifanya kama serikali. Kuna mkanganyiko miongoni mwa Wakenya na ukosefu wa uwajibikaji kwa sababu hakuna tofauti kati ya upinzani na serikali. ," Ruto alisema.

"Watu wenye tamaa ambao walipaswa kutekeleza majukumu yao kwa upande kinzani wa serikali wanaamua kuja na kuwa makachero na mabwanyenye serikalini."

Katika taarifa yake kuhusu uhaba wa mafuta nchini, Naibu rais Ruto alilaumu utekaji nyara wa serikali, akisema kuwa mashirika na maafisa wa umma wasio na tajiriba ya kufanya kazi wameshirikiana kuibia Wakenya.

Alisema Wakenya sasa wanasubiri hatua kutoka kwa wizara ya Hazina ya Kitaifa, Kilimo na Petroli.

Ruto alisisitiza kuwa kimya kutoka kwa wizara husika huku hali ikizidi kuwa mbaya ni jambo la kutia wasiwasi.

"Mtazamo wa kawaida na wa kutojali masaibu ya mamilioni ya Wakenya wanaotatizika ni jambo la kusikitisha na ambalo limeyapa ujasiri mashirika ambayo yamechukua sekta muhimu za kiuchumi kuwanyanyasa wakenya," Ruto alisema.

"Wapi hazina ya Shilingi bilioni 39 ya ruzuku ya mafuta iinayolenga kutatua shida kama hii?"

Aliongeza kuwa maafisa wa serikali hawapaswi kulaumu mgogoro wa Urusi na Ukraine kwa uhaba wa sasa wa mafuta.