Wazee wa Kalenjin wamwomba msamaha Raila kufuatia shambulio la ndege yake

Muhtasari

•Wazee hao wamesema baada ya siku 40 wataandaa ibada ya maombi na utakaso katika eneo ambalo kisa hicho kilitokea. 

•Wazee hao walisema hawawezi kuunga mkono visa kama hivyo na kuwataka Wakenya kudumisha amani na umoja katika kipindi cha uchaguzi.

Wazee wa Kalenjin karibu na eneo ambapo kisa cha chopper kilitokea Kabenes kaunti ya Uasin Gishu mnamo Aprili 5 2022
Wazee wa Kalenjin karibu na eneo ambapo kisa cha chopper kilitokea Kabenes kaunti ya Uasin Gishu mnamo Aprili 5 2022
Image: MATHEWS NDANYI

Wazee wa jamii ya Kalenjin wamemwomba radhi waziri mkuu wa zamani Raila Odinga kufuatia kisa cha kupigwa mawe kwa chopa yake katika eneo la Kabenes, kaunti ya Uasin Gishu.

 Wazee hao wamesema baada ya siku 40 wataandaa ibada ya maombi na utakaso katika eneo ambalo kisa hicho kilitokea. 

"Kwa mujibu wa mila zetu, familia ya Kibor bado inaomboleza na hatuwezi kufanya chochote kwa sasa hadi baada ya siku 40", alisema mzee mwingine Paul Tanui arap Tumbo.

Eneo la tukio lipo Kabenes karibu na nyumba ya Mzee Jackson Kiprotiich Kibor ambaye alizikwa siku ya Jumamosi. 

Odinga alikuwa amehudhuria mazishi hayo na alikuwa akiondoka wakati kundi la vijana lilizunguka chopa yake na kuipiga kwa mawe. 

Vijana 17 wamefikishwa mbele ya mahakama kuhusu kisa hicho huku mbunge wa eneo hilo Caleb Kostany, mwenzake wa Kapseret Oscar Sudi na spika wa bunge la Uasin Gishu David Kiplagat pia wakirekodi taarifa mjini Nakuru kuhusu kisa hicho.

 Msemaji wa baraza la wazee wa Kalenjin katika kaunti ya Uasin Gishu, Edwin Chepsiror aliwaongoza wazee ambao walitembelea nyumba ya Kibor na eneo la tukio hilo la Jumamosi.

Wazee hao walisema hawawezi kuunga mkono visa kama hivyo na kuwataka Wakenya kudumisha amani na umoja katika kipindi cha uchaguzi. 

"Tunaomba msamaha kwa Odinga na tunatumai atakubali tulichosema kwa sababu yeye pia ni mzee kama sisi", Chepsiror alisema. 

Alisema Odinga ni kiongozi anayeheshimika nchini na hakustahili kushambuliwa kwa namna hiyo.

 "Katika mila za kalenjin, kilichotokea ni chukizo. Tulikuwa tumekuja hapa kuomboleza na hakuna mtu anayepaswa kushambuliwa na kuumizwa wakati wa maziko", Chepsiror alisema. 

Alisema baada ya siku 40 watakutana katika eneo hilo kwa ajili ya kulitakasa kwa kufanya matambiko ili yasirudiwe tena.

 Mzee mwingine David Singo'ei alisema wao kama wazee hawakufahamu mpango wowote wa kumshambulia Odinga.

 Alisema viongozi wanaohusishwa na tukio hilo walihubiri amani wakati wa mazishi na wasingeweza kupanga tukio la aina hiyo. 

"Tunaiomba serikali kuchunguza ipasavyo tukio hilo na kuhakikisha waliohusika wanafikishwa mahakamani", alisema. 

Singo'ei alisema Odinga na viongozi wengine wote wako huru kufanya kampeni katika eneo hilo la bonde la ufa wakati wowote.

Wazee hao wamewataka vijana kutokubali kutumika kufanya vurugu wakati wa kampeni zinazoendelea.

 Pia wamewataka wanaowania viti vya kisiasa kutotumia vijana vibaya au kuwachochea Wakenya kufanya vurugu.

 "Nchi yetu lazima ibaki na amani wakati na baada ya uchaguzi," arap Tumbo alisema.