Matiang'i: Tukio la ndege ya Raila kupigwa mawe lilipangwa na kufadhiliwa

Muhtasari

• Waziri wa usalama wa ndanio Dkt Fred matiang'i aliiambia kamati ya bunge ya usalama wa taifa kwamba tukio la ndege ya Raila Odinga kupigwa mawe lilipangwa na kufadhiliwa na baadhi ya viongozi.

Ndege ya Raila Odinga ilishambuliwa kwa mawe katika kaunti ya Uasin Gishu Ijumaa
Ndege ya Raila Odinga ilishambuliwa kwa mawe katika kaunti ya Uasin Gishu Ijumaa
Image: FACEBOOK// RAILA ODINGA

Waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i anasema kwamba uvamizi wa mawe kwa ndege ya kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga wiki jana huko bonde la ufa ulikuwa umeratibiwa, kupangwa na hata kufadhiliwa na baadhi ya viongozi wa eneo hilo.

Akizungumza jana katika majengo ya bunge la kitaifa mbele ya kamati ya usalama wa kitaifa, Matiang’i alisema kwamba ana uhakika na maneno yake hayo na wala hapimi neno lolote kwani washukiwa zaidi ya kumi ambao kufikia sasa wametiwa mbaroni walipatika na baadhi ya vitu vinavyodhihirisha hilo pasi na kupepesa jicho.

Waziri huyo mwenye msimamo mkali aliiambia kamati hiyo kwamba uchunguzi umebaini kulikuwepo na mikutano kadhaa kati ya wanasiasa fulani na vijana hao katika harakati za kupanga shambulio hilo la mawe dhidi ya msafara wa Raila Odinga.

Matiang’i alisema washukiwa hao walinaswa na noti za shilingi hamsini kwa wingi, jambo linalodokeza uwezekano mkubwa kwamba shambulio dhidi ya Raila Odinga lilikuwa limefadhiliwa.

“Tukio lile lilipangwa kwa sababu tumekamata washukiwa wenye pesa nyingi, noti za 50. Ni wazi, lazima kulikuwa na mpangilio fulani nyuma ya hilo kwa sababu haingetokea jinsi ile kwamba washukiwa walikuwa na pesa nyingi zote zikiwa katika kiasi sawa cha noti za, na baadhi yao walikuwa wakizisambaza wakati huo huo,” Matiang’i alitetea uchunguzi wa polisi.

Waziri Matiang’i pia alisema viongozi wanaowania nyadhifa za kisiasa nchini wameanza hulka ya kuwatumia vijana kuzua vurugu dhidi ya wapinzani wao kwa kuwanunua kwa peni chache zaidi hata kuliko zile ambazo Yudas alimuuza Yesu.

"Wanasiasa wanatumia pesa kuwalipa vijana na kuhamisha vikundi vikubwa vya watu na kuwavusha wengine usiku. Jambo hili la kukodi umati wa watu na kujaribu kujitafutia umaarufu au kile unachoweza kukiita ushabiki wa kujifanya ndio utatuumiza,” alisema waziri Matiangi’.

Uvamizi na uharibifu wa ndege ya Raila Odinga ulitokea wiki iliyopita katika baada ya hafla ya mazishi ya mfanyabiashara na mkulima Jackson Kibor aliyefahamika na wengi kama mwenyekiti wa vuguvugu la watetezi wa haki za kiume.