Alfred Mutua kuungana na Ruto?

Muhtasari

• Mutua amesema kwamba kuna siri nyingi katika muungano wa Azimio ambazo zinamfanya kukosa imani na vuguvugu hilo.

• Amedokeza kwamba yupo tayari kushirikiana na naibu rais William Ruto.

Gavana wa kaunti ya Machakos ambaye pia ni kinara wa chama cha Maendeleo Chapchap, Aflred Mutua amesema kwamba hana imani tena na vuguvugu la Azimio.

Akizungumza katika mkutano na wajumbe wa chama hicho, Mutua alisema kwamba mpaka sasa hajaweza kufahamu maelezo yoyote yaliyopo katika makubaliano waliyotia saini ndani ya muungano huo.

Mutua alisema kwamba kuna ishara tosha kwamba chama chake hakitakikani katika muungano wa Azimio.

Kiongozi huyo alisema kwamba wagombea wa vyama vitatu vikuu ndani ya muungano huo [ ODM, Jubilee na Wiper] tayari wanapewa hela za kufanikisha kampeni zao huko wagombea wa chama chake wakiachwa mkono mtupu

Aidha, alishikilia kwamba hana chuki na naibu rais William Ruto na kwamba hana tatizo kushirikiana naye ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Alisema kwamba atafanya mkutano wa viongozi wakuu chamani [NEC] na kusikiliza maoni ya wanachama halafu baadaye atatoa uamuzi rasmi kuhusu mrengo atakaoungana nao.

"...Sitaki niingie mahali halafu siku chache nikipiga simu haichukuliwi, lazima tujipange vizuri," Mutua alisema.

Kiongozi huyo alishikilia kwamba ili kushirikiana na Raila Odinga lazima kuwepo na mfumo wa wazi kuhusu jinsi watakavyoshirikiana kuunda serikali baada ya uchaguzi wa Agosti 9.

Kauli ya Mutua inajiri siku moja baada ya gavana wa Makueni Kivutha Kibwana kutoa madai sawia ya kutengwa katika mikakati na mipango ya vuguvugu la Azimio la Umoja.