Kalonzo aongeza mchanganyiko zaidi ndani ya Azimio baada ya Wiper kumteua Ben Mulwa kuwania ugavana Nairobi

Muhtasari

• Chama cha Wiper kimemteua Ben Mulwa kuwania ugavana Nairobi na hivyo kukoleza mfarakano katika muungano wa Azimio ambapo pia Jubilee na ODM wanalenga kutoa mgombeaji wa nafasi hiyo.

• Mulwa atamenyana na Richard Ngatia, Agnes Kagure, Ann Kananu wote wa Jubilee, Tim Wanyonyi wa ODM katika kinyang'anyiro hicho. Ikumbukwe wote hawa wamo ndani ya muungano wa Azimio la Umoja.

• Hata hivyo baada ya Mike Sonko kujiunga na Wiper, wengi walidhani ni yeye angepewa tiketi ya kujaribu kukirudia kiti hicho alikong'atuliwa mwaka 2020.

Kinara wa Wiper kalonzo Musyoka na mgombea ugavana mteule wa Wiper Ben Mulwa
Kinara wa Wiper kalonzo Musyoka na mgombea ugavana mteule wa Wiper Ben Mulwa
Image: Twitter

Vuguvugu la Azimio la Umoja linazidi kukumbwa na nyufa kali wiki chache tu baada ya vyama vya kisiasa zaidi ya 17 kuungana ili kubuni muungano huo na kumteua kinara wa ODM Raila Odinga kama mgombea wake wa urais.

Nyufa na mifarakano ya ndani kwa ndani imekuwa ikiripotiwa huku ikisemekana kwamba vyama vingi ndani ya muungano huo vinataka kuwasilisha wagombeaji katika nyadhifa mbalimbali za kisiasa, jambo ambalo mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora alionya kwamba migawanyiko hiyo huenda itasababisha muungano wa Azimio kupoteza viti vingi kwa muungano pinzani wa Kenya Kwanza unaoongozwa na naibu rais William Ruto.

Kwa mfano katika kaunti ya Nairobi, wawaniaji wa kiti cha ugavana ni zaidi ya mmoja kutoka vyama zaidi ya vitatu vilivyomo ndani ya muungano wa Azimio la Umoja.

Richard Ngatia, Agnes Kagure na Ann Kananu wote wa Jubilee wanalenga ugavana wa jiji kuu, nafasi ambayo pia inamezewa mate na mbunge wa Westlands, Tim Wanyonyi anayesimama na chama cha ODM, na pia Wiper Alhamis kimemteua Ben Mulwa kuwania ugavana Nairobi, wote hawa wakionekana kutokubali kumwachia mmoja wao katika mwavuli wa Azimio la Umoja.

Chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka ndicho kimekuwa cha hivi punde kutangaza mgombea wao wa ugavana Nairobi ambapo aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi City Hall wakati wa utawala wa gavana Mike Sonko, Ben Mulwa ametangaza kupitia Twitter yake kwamba amepewa tiketi ya kuwakilisha chama hicho katika kinyang’anyiro hicho.

“Leo nimethibitishwa rasmi kuwa mgombea pekee wa Wiper katika kiti cha Ugavana, Kaunti ya Jiji la Nairobi, Safari yetu imekuwa ndefu na ngumu, lakini wakati umefika wa kuanzisha sura mpya katika usimamizi wa mji mkuu wa Kenya,” aliandika Mulwa.

Uteuzi wa Mulwa hata unakanganya zaidi kwani wengi walikujwa wanatarajia gavana aliyeng’atuliwa madarakani Mike Sonko ndiye angepatiwa tiketi hiyo, haswa baada ya kukigura chama tawala cha Jubilee na kuingia Wiper ambapo hapo awali alisisitiza mara kadhaa kwamba atakuwa debeni kuwania kiti hicho alichong’atuliwa miaka miwili iliyopita.

Awali, gavana wa Makueni profesa Kivutha Kibwana alionesha wazi kutofurahishwa kwake na matukio ndani ya muungano wa Azimio la Umoja ambapo alisema kuna madharau yameanza kuonekana kutoka kwa baadhi ya vyama vinavyojona vikubwa kuliko vingine.

Hili timbwiri linazidi kuchemka kama mvinyo wa kiasili unaotokwa na povu, cha msingi ni kukaa kitako, chukua njugu zako sote tusubiri jinsi matukio yatakavyojieleza yenyewe, iwe kwa picha, video au maneno!