Mudavadi ataka IEBC kusalia huru na kukataa muingilio

Muhtasari

• Mudavadi ameitaka tume ya IEBC, kutumia uhuru wake kikatiba pamoja na maadili chini ya sheria za uchaguzi kuandaa uchaguzi ulio wa haki, huru na kweli.

 

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Image: Musalia mudavadi/TWITTER

Kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi ameitaka tume huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, kutumia uhuru wake wa kikatiba pamoja na maadili chini ya sheria za uchaguzi kuandaa uchaguzi ulio wa haki, huru na kweli utakaodhihirisha haki ya kidemokrasia ya kila mkenya na kukomaa kwa demokrasia nchini Kenya.

Mudavadi akizungumza alipokutana na viongozi na wawaniaji wa viti mbali mbali chini ya Vyama vya ANC, UDA na Ford-K siku ya Ijumaa  jijini Nairobi, alisema kuwa tayari mahakama ya upeo kupitia uamuzi wa BBI imedhihirisha uhuru wa taasisi kuu, pasi na madai ya kuwepo kwa “DEEP STATE” na ikatoa uamuzi ulioambatana na sheria na sauti ya Mkenya ikasikika.

“Mkikaa tu na mkue wagumu na mjue mnalenga wapi kura yenu, mjue hakuna mtu ataharibu kura yenu. Na ile dalili imeonyeshwa na supreme court na korti zote, sasa tunataka pia wale wa IEBC wawe na motisha na wasitingisike kwa kuwa korti imeonyesha tayari, sasa tunataka IEBC nayo isitingisike na wewe mwanachi pia usitingisike ili tupige kura na tupate ushindi.” Musalia alisema.

Mudavadi kwenye hotuba yake kwa kundi hilo lilojumuisha viongozi kutoka maeneo bunge ya Embakasi Central, Embakasi North na Kasarani, amewataka wakenya kulinda kura zao baada ya kuzitumbukiza kwenye debe mnamo Agosti 9 akisema kuwa kulinda kura ni haki ya kila mkenya ya kidemokrasia huku akionya wenye nia ya kuhitilafiana na mkondo wa mambo kwenye debe la Agosti kwamba watakula huu na hasara juu.

Mudavadi amewataka wakenya kutokubali kupokea vitisho vya aina yeyote kuhusiana na jinsi kura ya Agosti 9 itakavyokwenda na kuwataka kujitokeza na kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia na linalolenga kuyabadilisha maisha ya wakenya.

“Hata kwa BBI kama wewe unasema ni Deep State walipigwa bao la kwanza na High Court, wakaenda kwa Court of Appeal wakapigwa bao lingine, Supreme Court wakiwa na hizo nguvu zao wakapigwa bao la tatu, Kwa hivyo nyinyi wananchi ndio deep state, mwananchi na kura yako wewe ndio deep state.” Alisema Musalia.

“Hakuna mambo ya kusema deep state deep state ati kila mtu ana nguvu hata Moi alikuwa na ushawishi mkubwa, alikuwa President na alikuwa amesekuma Uhuru kama project na alikuwa na ushawishi kama amiri jeshi mkuu wa majeshi yote lakini wakenya waliamua wanamtaka Kibaki na project ya Moi, Uhuru, ikaanguka. Sasa wembe ni ule ule, Uhuru ni rais na yeye ni mkuu wa majeshi lakini kikatiba na kwa kura, uamuzi wa mwananchi ni mkubwa kushinda yale mambo yako na mammlaka yako ya cheo,” aliongeza.

Mudavadi alisema kuwa yuko tayari kufanya kile awezalo katika safari yake ya kisiasa, ili raundi hii maisha ya wakenya yabadilke na utabiri wake ni kwamba ushindi wa Kenya Kwanza utakuwa ufunguo wa mlango wa mwamko mpya wa kukombolewa kwa wakenya wote.

“Kile ambacho nimesema sitaki ni kushurutishwa na kuambiwa kupiga magoti, na kwa niaba yenu nimekataa kupiga magoti, so you must also go there. Na hata kwa sasa kuna vijana wetu wasomi and they are sitting on the fence wanabahatisha kuona upepo unaenda upande gani, na siku Kenya Kwanza itachukua serikali ndio utaona wakikimbia hapa na sahizi hawataki kutusaidia tukipambana.”