Bishop Wanjiru ajiondoa kwenye kinyang'anyiro cha ugavana Nairobi, kumuunga mkono Sakaja

Muhtasari

•Karen Nyamu pia alijiuzulu nafasi yake ya useneta na sasa atamuunga mkono Seneta maalum Millicent Omanga kuwania kiti hicho.

Image: FACEBOOK//BISHOP MARGARET WANJIRU

Askofu Margaret Wanjiru wa kanisa la Jesus is Alive Ministry ametangaza kuwa ameacha azma yake ya kuwania kiti cha Ugavana wa Nairobi.

Wanjiru alitangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho ili kumwachia Seneta Johnstone Sakaja ambaye sasa ndiye atakayepeperusha bendera ya UDA.

Alikuwa anazungumza baada ya mkutano ulioandaliwa katika makazi rasmi ya DP Ruto mtaani Karen. Wanjiru sasa atawania useneti kwa tikiti ya UDA.

"Ninataka wafuasi wetu na wanachama wote wa chama waelewe, na hata viongozi wetu wengine wote wa chama waelewe kwamba muungano huja na changamoto kadhaa. Na mojawapo ya changamoto hizo ni kwamba lazima kuwe na kupewa na kupokonywa," Wanjiru alisema.

Katika matamshi yake, Sakaja alimsifu Wanjiru kwa kuchukua uamuzi huo mkubwa wa kujiuzulu na kuunga mkono azma yake.

Karen Nyamu pia alijiuzulu nafasi yake ya useneta na sasa atamuunga mkono Seneta maalum Millicent Omanga kuwania kiti hicho.