Spika Justin Muturi ajiunga na muungano wa DP Ruto wa Kenya Kwanza

Muhtasari

•Spika Muturi alisema uamuzi wake wa kujiunga na muungano huo ni baada ya kushauriana na wanachama wa chama chake na viongozi wa jamii.

•DP kwa upande wake alimkaribisha Spika kwenye chama akisema ajenda yake na ya Kenya Kwanza zinawiana.

Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Spika Justin Muturi wakati wa kikao na wanahabari katika Klabu ya United Kenya Nairobi Jumanne 11, Januari.
Image: WILFRED NYANGARESI

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amejiunga na Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na naibu wa rais William Ruto.

Chama cha Spika cha DP  kilitia saini mkataba wa muungano na Kenya Kwanza siku ya Jumamosi katika hoteli  iliyo Karen,  jijini Nairobi.

Waliohudhuria utiaji saini huo ni Ruto, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang'ula miongoni mwa wanasiasa wengine. Wabunge wengi wanaomuunga mkono Ruto walikuwepo.

Spika Muturi alisema uamuzi wake wa kujiunga na muungano huo ni baada ya kushauriana na wanachama wa chama chake na viongozi wa jamii.

"Nina furaha kwamba baada ya mazungumzo kadhaa kuhusu kuja pamoja, leo tumetambua ndoto hiyo ya kufanya kazi pamoja kwa watoto wetu na watoto wa watoto wetu," Spika Muturi alisema.

Aliongeza: "Nimesafiri katika maeneo mengi ya nchi na ninaweza kuthibitisha kwamba mapigo ya moyo ya Wakenya wengi yanaambatana na matamanio ninayoshikilia katika muungano huu. Tuna furaha kujumuika na muungano huo".

Aliendelea kukemea serikali ya sasa akisema halitalazimisha taifa zima kuelekea mwelekeo fulani wa kisiasa.

DP kwa upande wake alimkaribisha Spika kwenye chama akisema ajenda yake na ya Kenya Kwanza zinawiana.

Alisema ajenda ya muungano wao ni kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya taifa.

"Tunajivunia asubuhi ya leo kuwa tumejumuika na Chama cha DP ambacho kinahusishwa na kubadilisha uchumi wa taifa hili. Ni hitimisho la miezi ya mashauriano makali yaliyopelekea kutiwa saini kwa mkataba wa muungano," alisema.

Mudavadi kwa upande wake alisema hatua hiyo ya Spika ni mwendelezo wa tangazo alilolitoa Januari katika chama chake cha NDC.

"Tuliposema kutakuwa na tetemeko la ardhi, hakika hili ni tetemeko jingine."

Habari za Spika Muturi kuhamia Muungano wa Kenya Kwanza zilisambazwa kwa mara ya kwanza na washirika wa DP mnamo Ijumaa.

Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot alikuwa wa kwanza kufichua kuwa spika ndiye aliyejiunga na Kenya Kwanza hivi punde.

"Usajili wa Hivi Punde. Kenya Kwanza FC. Tunamaanisha biashara," alisema kwenye tweet iliyokuwa na taswira yake na Spika Muturi Jumamosi asubuhi.

Spika Muturi, ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Democratic Party, alikuwa ametangaza nia ya kuwa rais wa tano wa Kenya.

Uamuzi wake wa kufanya kazi na DP unazua shaka iwapo atadumisha ndoto yake ya urais au atachagua kumuunga mkono Ruto.

Matukio hayo yanakuja siku ya makataa ya vyama vya siasa kuwa wanachama wa chama cha siasa cha muungano.