Balaa katika Azimio huku OKA ikipinga usajili wa Muungano

Muhtasari

•Miongoni mwa mambo matatu ambayo timu ya OKA inataka kushughulikiwa ni pamoja na suala la mgombea mwenza ambalo ripoti zinasema huenda kuna mipango yao kuchengwa.

•Yanajiri takriban wiki moja baada ya vyama vinane ambavyo ni wanachama wa Azimio kutishia kujiondoa iwapo malalamishi yao hayatasikilizwa.

Mkuu wa Azimio la Umoja One-Kenya, Kalonzo Musyoka akiwaonyesha wakuu wachache Raila Odinga jambo kwenye simu yake wakati wa mkutano wa kampeni huko Turkana, Aprili 4, 2022.
Kalonzo na Raila Odinga Mkuu wa Azimio la Umoja One-Kenya, Kalonzo Musyoka akiwaonyesha wakuu wachache Raila Odinga jambo kwenye simu yake wakati wa mkutano wa kampeni huko Turkana, Aprili 4, 2022.
Image: TWITTER// RAILA ODINGA

Azimio One Kenya ipo katika njia panda baada ya sehemu ya Muungano huo kumwandikia Msajili wa Vyama vya Kisiasa wakitaka kusimamisha usajili wa muungano huo mara moja.

Mrengo wa One Kenya Alliance ambao unaoleta pamoja Wiper Party inayoongozwa na Kalonzo Musyoka,KANU inayoongozwa na Gideon Moi na United Democratic Party yake Cyrus Jirongo unalenga kusitisha shughuli ya usajili hadi masuala fulani yatatuliwe.

Miongoni mwa mambo matatu ambayo timu ya OKA inataka kushughulikiwa ni pamoja na suala la mgombea mwenza ambalo ripoti zinasema huenda kuna mipango yao kuchengwa.

"Pingamizi letu linatokana na ukweli kwamba masuala matatu (3) hayajaafikiwa na yanapaswa kujadiliwa na kuafikiwa kabla ya Mkataba huo kusajiliwa kikamilifu," OKA ilisema.

Timu ya OKA inahoji kuwa nafasi ya mgombea mwenza ni hifadhi ya Kalonzo na sasa wanahofia kwamba wanaweza kuipoteza ikiwa mipango ya sasa itaenda kama ilivyo.

Timu ya OKA pia inadai kuwa kuna makubaliano mapya ya muungano ambayo yamewekwa kwa Msajili wa Vyama, jambo ambalo wanahofia kuwa linaweza kuhatarisha maslahi yao kwenye kikosi hicho.

OKA wakati huo huo inashikilia kuwa Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya ni zao la vyama vitatu vikuu ambavyo ni pamoja na ODM, Jubilee na Wiper.

Wanahoji kuwa kuongezwa kwa nguzo ya nne katika muungano huo kunamaanisha kuwa makubaliano ya awali yametengwa, hatua inayohatarisha maslahi yao.

Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya vyama vinane ambavyo ni wanachama wa Azimio kutishia kujiondoa iwapo malalamishi yao hayatasikilizwa.

Miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa na vyama hivyo 8 ni pamoja na kujumuishwa kwa nguzo ya nne kwenye muungano, jambo ambalo timu ya OKA sasa pia imepinga

Timu hiyo ilitishia kujiondoa Azimio endapo malalamiko yao hayatatuliwa.

Malalamiko hayo yalishuhudia kinara wa ODM Raila Odinga akiitisha mkutano wa dharura ambao ulifanikisha malalamishi yao kutatuliwa.

Vyanzo vya habari vinasema huenda vyama hivyo8 viliongezwa kuwa nguzo ya nne ya muungano na makubaliano ya awali ya muungano yakafanyiwa marekebisho ili kuafiki mabadiliko hayo, kinyume na matakwa ya OKA.

Mnamo Jumamosi, Kalonzo alisema kuwa ataridhika na wadhifa wowote au jukumu ambalo atapewa katika Azimio.

“Nataka ndugu yangu Raila ajue, muundo wowote watakaokuja nao, mifumo yoyote ya kisiasa, huu ndio wakati wa Raila Odinga kuwa rais wa Kenya,” Alisema