"Ni Handshake!" Mgombea MCA Kisumu aunda bango moja lenye UDA na Raila Odinga

Muhtasari

• Mgombea ujumbe wa kaunti katika wadi  ya Kisumu ya Kati amezua gumzo baada ya kuunda bango lenye nembo ya Ruto na Raila

Bango lenye nembo za UDA na Raila kwa pamoja
Bango lenye nembo za UDA na Raila kwa pamoja
Image: Twitter//Rodgers Kipembe

Pameibuka maoni kinzani na mjadala mkali katika mitandao ya kijamii baada ya bango la mwanasiasa anayelenga kuwania kiti cha ubunge wa kaunti kwa tiketi ya chama cha naibu rais William Ruto, UDA, kuzuka likiwa na nembo za UDA na ile ya Raila ambaye ni wa Azimio la Umoja.

Picha hiyo iliyopakia kwenye mtandao wa Twitter na katibu mkuu wa chama cha NOPEU Kenya, Rodgers Kipembe Mpuru inaonesha mwanasiasa huyo ambaye jina moja tu ndilo linaonekana, MUSA anayelenga kuwa mjumbe wa Kisumu ya Kati kupitia chama cha UDA.

Bwana MUSA katika bango lake ambayo ameifanya vizuri tu tena kwa ustadi wa hali ya juu huku akiweka nembo na rangi zinazokitambulisha chama cha UDA alimalizia chini pembeni kulia mwa nembo yake na nembo ya kinara wa ODM Raila Odinga ambayo wengi wanaitambua kama nembo ya herufi moja kubwa ya ‘R’

Hili limezua mjadala mkali mitandaoni huku baadhi wakimtetea kwamba alilazimika kufanya hivo kama njia moja ya kuwatongoza wafuasi sugu wa Raila hata kama anatumia chama cha hasidi wake wa Kisiasa, William Ruto katika eneo ambalo ni kitovu cha uungwaji mkono cha Raila.

Wengine walitania kwamba huenda nembo hiyo yenye herufi ‘R’ japo inajulikana kuwa ya Raila, pengine MUSA au fundi aliyemtengenezea bango hilo aliitafsiri kusimamia jina la kinara wa UDA, William Ruto ambaye pia jina lake la pili linaanza na herufi hiyo ya ‘R’

Wakenya hawaishiwi na vituko bwana!