Rais Kenyatta wakutana na naibu wake William Ruto katika hafla Murang'a

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta wanatarajiwa kukutana uso kwa uso na naibu wake William Ruto katika hafla moja kaunti ya Murang'a

• Mkutano huu unakuja wiki chache tu baada ya wawili hao kutupiana cheche kali baada ya Kenyatta kumuunga mkono Raila Odinga kuwa mrithi wake.

Rais Uhuru Kenyatta, William Ruto
Rais Uhuru Kenyatta, William Ruto
Image: MAKTABA

Alhamis 14, rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanatarajiwa kukutana tena katika hafla ya kidini pamoja kwa mara ya kwanza tangu kutokea kwa handshake 2018 baina ya rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, Handshake ambayo ilichangia urafiki wa rais na naibu wake kusambaratika.

Kulingana na ripoti kutoka wandani wa wawili hao, naibu wa rais William Ruto atafanya ziara ya kisiasa katika kaunti ya Murang’a baada ya hafla ya kidini katika kanisa la AIPCA, Gakarara, hafla ambayo pia rais Kenyatta anatarajiwa kuhudhuria.

Kukutana kwa wawili hao kumezua mjadala mkali mitandaoni kukiibuliwa maoni kinzani kuhusu kanisa kuwakutanisha wawili hao kwa mara ya kwanza tangu uhusiano wao kuzorota huku wakionekana pamoja mara moja moja tu wakati wa hafla za kitaifa ambapo wanaonekana kama kukutana huko kunakuwa kwa kulazimisha tu bali si hiari.

Haijajulikana kama wawili hao watasalimiana au hata kuzungumza pamoja ikizingatiwa kwamba katika siku za hivi karibuni wawili hao wametoka nyuma ya pazxia na kutupiana cheche peupe huku rais akimtuhumu naibu wake kuwa anadanganya watu wa kanisa mpaka kusema kanisa nao wanakosea kukubali pesa ambazo Ruto anapeleka huko kama michango.

Rais pia mwezi uliopita alimtuhumu naibu wake kwa kufanya njama ya kumng’atua mamlakani jambo ambalo Ruto alijibu kiume kwa kumkashfu vikali rais kwamba anajaribu kuwapotosha wakenya.

Mbunge wa Kandara Alice Wahome ambaye ni mwandani wa Ruto alidhibitisha hilo na kusema kwamba atakuwepo katika eneo hilo ili kumkaribisha rais Kenyatta.

Macho na maskio ya wakenya sasa yanasubiri kuona na kusikia iwapo wawili hao watazungumza pamoja, wiki kadhaa baada ya kutupiana maneno.