Isaac Mwaura apinga matokeo ya mchujo huko Ruiru

Muhtasari

• Seneta mteule Isaac Mwaura amepinga matokeo ya kura za mchucho  za UDA kwa kiti cha ubunge cha Ruiru.

• Matokeo ya muda yalionyesha kuwa Ng'ang'a alipata kura 4,688 akifuatiwa na Mwaura aliyepata 2,428.

 

Seneta Mteule Isaac Mwaura
Seneta Mteule Isaac Mwaura
Image: MAKTABA

Seneta mteule Isaac Mwaura amepinga matokeo ya kura za mchucho  za UDA kwa kiti cha ubunge cha Ruiru.

Mshindani wa Mwaura Simon Ng'ang'a aliongoza katika uteuzi wa UDA, licha ya kuwa uteuzi wake haujakamilika katika vituo vitatu vya wadi ya Mwiki.

Matokeo ya muda yalionyesha kuwa Ng'ang'a alipata kura 4,688 akifuatiwa na Mwaura aliyepata 2,428.

Akizungumza na wafuasi wake Ijumaa asubuhi, Mwaura alisema zoezi hilo si la haki na kutaka lirudiwe.

“Huu uchanguzi tunasema urudiwe [Uchaguzi urudiwe],” Mwaura alisema alisema.

Aliongeza kuwa wanachama hao hawatamruhusu mwanachama aliyeondoka Jubilee kutatiza zoezi la upigaji kura.

"Tumekijenga chama hiki, tunajua machungu," aliongeza.

Aidha, alimtaka Naibu Rais William Ruto kusuluhisha suala hilo na kuagiza zoezi hilo kuandaliwa upya.

Alisema kuwa si haki majina ya wasio wanachama wa UDA kuorodheshwa mbele ya wanachama asili  wa UDA kwenye karatasi za kupigia kura.

"Kabogo aliondoka UDA, mbona jina lake linaonekana kwanza kwenye karatasi?" Mwaura aliuliza.

Wafuasi wa Mwaura wamekariri kuwa uchaguzi unapaswa kufanywa upya. "Tunafaa kuruhusiwa kumpigia kura mgombea tunayemtaka," walisema.

Simon Waiharo, ambaye pia anawania tiketi hiyo, alikariri kuwa mchakato huo unapaswa kurudiwa kwa uwazi.

Ng'ang'a amewapongeza wakaazi kwa kujitokeza kupiga kura na kuonyesha imani katika ushindi wake.

"Nawashukuru wakazi wa Ruiru kwa kujitokeza kunipigia kura. Ingawa sijatangazwa mshindi kutokana na changamoto zilizotokea Mwiki, naamini bado nitafanikiwa mwishowe," Ng'ang'a alisema.

Mwaura alipoteza azma yake ya ubunge katika uchaguzi Mkuu wa 2017 kwa Ng'ang'a.