Kalonzo adai Ruto aliiba kura 2013 na 2017 bila rais Kenyatta kujua

Muhtasari

• Kalonzo Musyoka aliibua madai kwamba naibu rais William Ruto aliiba chaguzi za 2013 na 2017 kwa ajili ya rais Kenyatta bila Kenyatta kujua njama hiyo.

Kalonzo Musyoka katika studio za Radio Jambo mnamo tarehe 1 mwezi Septemba
Kalonzo Musyoka katika studio za Radio Jambo mnamo tarehe 1 mwezi Septemba
Image: ANDREW KASUKU

Kinara wa chama cha Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka ambaye pia ni mmoja wa viongozi wakuu katika muungano wa Azimio-One Kenya kwa mara nyingine ameibua mapya tena baada ya kudai kwamba naibu rais William Ruto aliiba kura za chaguzi kuu 2013 na 2017 kwa kumpendelea rais Uhuru Kenyatta bila rais mwenyewe kujua.

Akizungumza wikendi iliyopita katika kaunti ya Kajiado, Musyoka alisema kwamba Ruto alifanya njama hiyo ya kuiba kura ili kumfanya Uhuru Kenyatta kuwa rais kwa awamu mbili lakini akamuepusha rais Kenyatta kutokana na madai hayo ya wizi kwa kusema kwamba Ruto alikuwa anafanya uahini huo pasi na Kenyatta kujua licha ya kwamba ni yeye alikuwa akiibiwa.

Kiongozi huyo wa muda mrefu kutokana Ukambani aliendelea kwa kumuonya naibu rais dhidi ya kuendeleza tabia yake ya kuiba kura katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti na kusema kwamba safari hii kuna timu yenye nguvu zaidi na ambayo itakuwa macho wakati wote kuzuia njama zozote za Ruto kufanya vile ambavyo alifanya katika chaguzi za awali.

Kalonzo Musyoka ambaye alionekana kumvalia njuga kweli kweli naibu rais William Ruto katika hafla hiyo pia alimzomea kwa kujifanya mwizi mtakatifu kama mwizi wa Uingereza, Robin Hood aliyekuwa akiibia matajiri na serikali huku akiwasaidia maskini.

Musyoka aliwarai watu wa jamii ya Maasai kuunga mkono muungano wa Azimio-One Kenya na kumfanya Raila kuwa rais wa tano wa Kenya kando na kuwataka wamuombee kuchaguliwa kama mgombea mwenza wa Raila.