Mimi ndiye rais wa wananchi-Jimi Wanjigi asema

Muhtasari
  • Hivyo aliwataka Wakenya kumuunga mkono  katika azma yake ya kugombea urais
Jimi Wanjigi akizungumza baada ya kujiunga na chama cha Safina 9/Machi/2022
Image: Ezekiel Aming'a

Mwaniaji urais Jimi Wanjigi amekariri kuwa jina lake litakuwa kwenye kura ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Agosti 9.

Akizungumza mjini Malindi, Wanjigi ambaye ni mgombeaji urais wa Chama cha Safina, alisema yeye ndiye rais wa wananchi kwa kuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga alikuwa akifanya kazi na serikali.

Hivyo aliwataka Wakenya kumuunga mkono  katika azma yake ya kugombea urais.

Wakati uo huo, Wanjigi alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuchukua kiti cha nyuma katika siasa za mrithi, akibainisha kuwa alihudumu vyema katika mihula yake miwili na hivyo anafaa kuondoka kwa amani.

"Alipigiwa kura kwa nia njema lakini sasa anajinufaisha kwa Wakenya kwa kujaribu kutawala kupitia mlango wa nyuma. Tunamtaka Uhuru Kenyatta arudi nyumbani kwa amani," alisema Wanjigi.

Wanjigi pia aliwashukuru wagombeaji wa Chama cha Safina kutoka ngazi ya ugavana hadi MCA, akibainisha kuwa chama hicho kitasimamisha mamia ya wagombea katika uchaguzi wa Agosti.

Aliwahakikishia Wakenya kwamba yuko kwenye kinyang'anyiro cha Urais hadi mwisho, akiongeza kuwa ataunda tu miungano ya moja kwa moja na watu wa Kenya.

Wanjigi alijitangaza kuwa rais halisi wa wananchi akisema nafasi hiyo iliachwa wazi baada ya Raila kufanya hendishekina  Rais Kenyatta.

“Mnaponiona hapa, mimi ndiye niliyechukua wadhifa wa Raila Amolo Odinga kama rais wa wananchi, Alienda Harambee House kufanya hendisheki na wengine na kuacha nafasi hiyo wazi,” Wanjigi alisema.