Uhuru:Kenya inamhitaji Raila ambaye ni mkomavu na asiye na ubinafsi

Muhtasari
  • Uhuru alikuwa akizungumza Ikulu alipokutana na viongozi wa Kiislamu kutoka kote nchini kwa ajili ya Iftar
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amewashauri Wakenya kuwachagua viongozi dhabiti wenye uwezo wa kuunganisha nchi kabla ya uchaguzi.

Uhuru alikuwa akizungumza Ikulu alipokutana na viongozi wa Kiislamu kutoka kote nchini kwa ajili ya Iftar.

Rais ambaye amemuunga mkono kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alisema Wakenya wanapaswa kumchagua kiongozi ambaye anaweza kusuluhisha changamoto zinazowakabili wananchi.

“Nataka kukuambia kujenga taifa si rahisi jinsi watu wengi wanavyofikiri. Si rahisi. Dhoruba ni nyingi na inahitaji Mkono thabiti sio mkono unaoangalia kila kitu kwa mtazamo wa ubinafsi. Sio mkono ambao badala ya kutafuta kutatua shida unatafuta mtu wa kulaumiwa.

“Sasa ikiwa unatafuta mtu wa kumlaumu badala ya kurekebisha tatizo unawezaje kuwa msuluhishi wa matatizo? Wewe ni kitambulisho cha tatizo. Na nchi hii inahitaji msuluhishi wa matatizo kwa sababu hakuna siku matatizo yatakoma, matatizo yataendelea kujitokeza."

Uhuru amewataka wakenya kuendelea kuliombea taifa lao wanapojiandaa kuwachagua viongozi ambao watajitahidi kutoa suluhu kwa matatizo.

“Kwa hivyo unahitaji watu ambao wako tayari kuvuta pamoja na kutatua matatizo kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya maendeleo ya nchi. Na ndio maana ninawaomba ndugu zangu Waislamu muda huu na katika mwezi huu Mtukufu, ninawaomba, tuwaombee amani na umoja,” alisema.

"Tunaomba kwamba tupate kiongozi ambaye atatuunganisha na kuendelea kushughulikia matatizo yetu."

Alipigia debe Raila akisema ndiye anafaa zaidi kurithi uongozi wa nchi kutoka kwake baada ya uchaguzi wa Agosti.

Alisema Raila alikuwa kiongozi wa kweli na mkomavu na mwenye mapenzi makubwa kwa nchi yake na rekodi ya uimara wa kisiasa.

“Nawaomba sote tuungane chini ya mwamvuli wa Azimio. Na ninapotazama kushoto au kulia, sioni mtu mwingine (mtu) ambaye ana uwezo wa kutuunganisha, ambaye ana uwezo wa kusamehe, ambaye ana uwezo wa kuwa mtulivu na mvumilivu zaidi ya Raila," alisema.

Niseme kujenga taifa si jambo la siku moja bali ni zoezi endelevu. Ni kile tunachokiita mbio za relay. Unakimbia na kukabidhi kijiti kwa mwenzako. Na Kenya iko hapa na itaendelea kustahimili hata baada ya sisi kupita kwa muda mrefu," alisema.

"Wengi wamekuwa nasi na wengi wameondoka na tunawashukuru kwa walichokifanya na mafanikio waliyoyapata."

Kuhusu maendeleo, Uhuru alidokeza kuwa Kenya imepata maendeleo makubwa katika miundombinu.

“Tuna amani, tumepata maendeleo kwa kadri tulivyofanya kazi pamoja. Tumeungana na wananchi wana uhuru na demokrasia ya kujieleza kwa uhuru na muhimu zaidi wana uhuru wa kuabudu,” alisema.