Hatimaye Isaac Mwaura akubali matokeo ya mchujo wa UDA na kumpongeza mshindi

Muhtasari

• Isaac Mwaura - Nimeamua kukubali matokeo. Hii ni kuhakikisha kuwa chama kinasalia kuwa na umoja na kuzingatia lengo letu la kuhakikisha kuwa Naibu Rais William Ruto anakuwa Rais wa 5 wa nchi yetu kuu.

Image: FACEBOOK// ISAAC MWAURA

Aliyekuwa akigombea ubunge wa Ruiru kupitia tiketi ya chama cha UDA, Isaac Mwaura hatimaye amekubali matokeo ya mchujo wa chaam hicho ambapo ameungana mkono na Simon Ng’ang’a ambaye alishinda tiketi hiyo.

Awali, Mwaura alikuwa amepinga matokeo hayo na kutaka uongozi wa chama hicho cha naibu rais William Ruto kufutilia mbali uchaguzi huo wa mchujo na kuuandaa upya baada ya Ng’ang’a kumbwaga na kushinda tiketi ya UDA ambapo sasa atamenyana na wagombea kutoka vyama vingine wanaolenga kuwakilisha wakaazi wa Ruiru katika bunge la kitaifa.

Akiungana na mshindi kwa kusherekea ushini huo, Mwaura alisema kwamba ni wakati sasa wa kuuguza maumivu ya kushindwa na pia kukubali maamuzi yaliyofanywa na wakaazi wa eneo hilo ambako amekuwa akizunguka kujumuika na wakaazi kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kuwazawidi baadhi ya vijana torori, ambazo ni nembo ya chama cha UDA.

“Nikiungana na mshindani wangu Simon Ng’ang’a leo katika kituo cha kuhesabia kura kituo cha Kist baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha ubunge cha Ruiru nilichowania sana. Ni wakati sasa wa kuponya majeraha makubwa kutoka kwa kura za mchujo za chama na hivyo kusonga mbele kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti,” aliandika Mwaura kupitia Facebook yake.

Mwanasiasa huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiteuliwa katika kamati za bunge kupigania na kutetea haki za watu wenye ulemavu wa Ngozi kama yeye alisema kwamba uamuzi wake wa kukubali matokeo ni kwa sababu ya kutaka umoja na uwiano wa chama cha UDA.

“Hii ni kuhakikisha kuwa chama kinasalia kuwa na umoja na kuzingatia lengo letu la kuhakikisha kuwa Naibu Rais William Ruto anakuwa Rais wa 5 wa nchi yetu kuu. Chama chetu na maadili yake ni makubwa zaidi kuliko yeyote kati yetu. Tukimtanguliza MUNGU tutashinda!! Nakushukuru!” aliandika Mwaura.