"Acha matakwa ya kipuuzi!" Seneta Ole Kina amzomea Kalonzo kutaka kuwa mgombea mwenza wa Raila

Muhtasari

• Seneta wa Narok Ledama Ole Kina amemtaka Kalonzo aache matakwa ya kipuuzi na badala yake kuwaonesha kura.

• Alisema mtu yeyote anayetaka kuwa mgombea mwenza wa Raila sharti aoneshe ubabe wake katika kuvutia kura.

LEDAMA 2
LEDAMA 2

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina amewasuta wale wanaong’ang’ania nafasi ya kuwa mgombea mwenza wa kinara wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga huku wakitoa masharti makali wakitaka kupewa hiyo nafasi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ole Kina aliwasuta vikali na kuwaambia waache vipindi kwani watu wenye fikira za kusonga mbele sasa hivi wanasakanya kura na si kutoa vitisho kuhusu nini watafanya iwapo watanyimwa nafasi ya kuwa mgombea mwenza wa Raila.

Akionekana kumtupia vumbi machoni kinara wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka ambaye amekuwa akitoa masharti makali akitaka kupewa nafasi hiyo, Ole Kina alimtaka awaoneshe kura na kumuambia kwamba wakenya wenye fikira za mbele hawatomsikiliza.

“Yeyote anayetaka kuwa mgombea mwenza wa Raila lazima atuoneshe ubabe wake kwa kuwavutia wapiga kura nchini kote kwa kutumia masuala yanayowakumba. Haya mambo ya kujihisi unafaa ni ushauri potofu. Tunataka watu wenye fikra za mbele, walio tayari kujitolea kwa Kenya, tuwache vipindi. Acha matakwa yako hayo ya kipuuzi. Tuoneshe kura. Wakenya wenye kusonga mbele hawatakusikiliza…sisi twasonga mbele,” aliandika Ole Kina.