Azimio la Umoja kuzindua mgombea wao wa ugavana kaunti ya Nairobi, Alhamisi - Tim Wanyonyi

Muhtasari

• Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi amefichua kuwa Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya utamtaja mgombea wake wa kiti cha ugavana wa Nairobi siku ya Alhamisi.

• "Muungano unashauriana  na tutatoa taarifa Nairobi Alhamisi hii. Uamuzi wa muungano huo utakuwa nyongeza au kupunguza azma yangu," Wanyonyi alisema.

Image: Douglas Okiddy

Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi amefichua kuwa Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya utamtaja mgombea wake wa kiti cha ugavana wa Nairobi siku ya Alhamisi.

Mbunge huyo ambaye pia anakodolea macho kiti cha ugavana, alithibitisha kuwa mazungumzo yanaendelea kuhusu nani atakuwa mgombea anayefaa.

"Muungano unashauriana  na tutatoa taarifa Nairobi Alhamisi hii. Uamuzi wa muungano huo utakuwa nyongeza au kupunguza azma yangu," Wanyonyi alisema.

Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari siku ya Jumanne, mbunge huyo aliwahakikishia wafuasi wake kwamba bado yuko kwenye kinyang'anyiro hicho na ana matumaini atapata tikiti hiyo.

"Uongozi ni wito na tangu mwanzo, huwa nasema 'si mimi ni sisi'. Bado niko kwenye kinyang'anyiro,"aliongezea.

Gazeti la The Star limebaini kuwa mbunge huyo wa Westlands alikuwa ameitwa katika Ikulu Jumanne asubuhi kuhusu mazungumzo kuhusu kinyang'anyiro cha kiti cha ugavana.

"Siwezi kuthibitisha kwa kina kuhusu mkutano huo lakini ninaweza kukuhakikishieni ni kuhusu siasa za Nairobi na kinyang'anyiro cha ugavana," chanzo ambacho hakikutaka kutajwa jina kiliiambia Star.

Wiki jana, Wanyonyi alikanusha madai kwamba alishawishika kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho baada ya kukutana na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Vile vile alipuuzilia mbali madai kwamba angepigwa kiwiko kutokana na idhini yoyote ya kisiasa ya Azimio kwa sababu Raila hawezi kuidhinishwa kuwania urais na wakati huo huo kuwa na mwaniaji kiti cha ugavana wa Nairobi.

Mwezi uliopita, Chama cha ODM kiliwahakikishia wawaniaji Nairobi kwamba hakuna tikiti za uteuzi ambazo zimetolewa kwa mgombeaji yeyote wa jiji.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alifichua kuwa mpango huo ulikuwa ni kwamba tikiti za uteuzi za chama hicho Nairobi zitolewe mara moja kwa wagombeaji wote.

Sifuna ambaye amekuwa akiunga mkono azma ya Wanyonyi kuwa gavana wa Nairobi alimhakikishia tikiti ya chama hicho.

Kwa miaka 15 iliyopita, Wanyonyi amehudumu Nairobi, kwanza kama diwani aliyependekezwa kati ya 2007 na 2013 na kisha kama Mbunge wa Eneo Bunge la Westlands tangu 2013 hadi sasa.

Mbunge huyo alikuwa amezindua rasmi azma yake ya kuwania kiti cha ugavana mwaka jana. Hatima ya Wanyonyi sasa iko katika uamuzi wa muungano huo.

Kwa upande wa Kenya Kwanza Alliance, Naibu Rais William Ruto alimzindua Seneta Johnson Sakaja kama mgombeaji wao wa kiti cha ugavana wa Nairobi.

Hii ilikuwa baada ya Askofu Margaret Wanjiru kuachana na azma yake ya ugavana na kumpendelea Sakaja na sasa atawania kiti cha useneta wa Nairobi.

Wanachama wengine wa Azimio wanaowania tikiti ya ugavana ni pamoja na Gavana wa Nairobi Ann Kananu, Mfanyabiashara Agnes Kagure na Aliyekuwa Chama cha Kitaifa cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda nchini (KNCCI) Richard Ngatia.

Image: Douglas Okiddy