Raila asutwa kwa kutaka Luo Nyanza kupiga kura 6-piece kwa ODM

Muhtasari

• Raila alizungumza katika mazishi ya aliyekuwa balozi wa Kenya kwenda Qatar na kuwataka watu kupiga kura 6-piece.

KInara wa ODM Raila Odinga
Image: George Owiti

Watu mbalimbali wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuzungumzia matamshi ya kinara wa muungano wa Azimio-One Kenya Raila Odinga kwamba anataka watu wapige kura kuchagua tu wagombea kupitia chama chake cha ODM pekee kutoka kura ya ugavana hadi ile ya udiwani.

Akizungumza Jumatatu katika hafla ya msiba wa aliyekuwa balozi wa serikali ya Kenya nchini Qatar, Paddy Ahenda nyumbani kwake katika kaunti ya Migori, Odinga aliwarai wakaazi wa kaunti hiyo kujitokeza kwa wingi Agosti 9 na kupiga kura kwa mgombea yeyote mwenye tiketi ya chama cha ODM bila hata kuangalia manifesto yake, bora tu ni wa ODM, maarufu kwa lugha ya kimombo kama 6-piece voting.

“Nataka watu wa eneo hili wapige kura 6-piece tu ili chama kiendelee kuwa na nguvu. Wacha MCA, mbunge, mwakilishi wa wanawake, seneta, gavana na rais watoke ODM,” aliwarai Wakaazi ambao walionekana kutofurahishwa na tamko hilo.

Hii ni mara ya kwanza chama cha ODM kinashuhudia ukaidi mkali kutoka kwa watu wa eneo pana la Luo Nyanza ambapo watu wengi wanaonekana kukataa kuchaguliwa viongozi kutokana na hatua ya chama hicho kutoa tiketi za moja kwa moja za ODM kuwania nyadhifa mbalimbali za siasa eneo hilo.

Kwa mfano kule Siaya, ODM ilitoa tiketi ya moja kwa moja ya ugavana kwa seneta James Orengo ambaye amepata pingamizi kali kutoka kwa wakaazi ambao hawamtaki lakini chama hicho kinamlazimisha kwa wananchi.

Hali ndio kama hiyo katika kaunti zingine kama Migori ambapo Ochilo Ayacko hatakikani licha ya kupewa tiketi ya moja kwa moja, Kisumu pia gavana wa sasa Anyang’ Nyong’o amepata upinzani mkali na kule Homabay alikokuwa akizungumza jana ODM ilimpa tiketi ya moja kwa moja mwakilishi wa kike Gladys Wanga kuwania ugavana ambapo amekabiliwa na upinzani mkali na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Evans Kidero anayewania ugavana huko kama mgombea huru baada ya kunyimwa tiketi ya ODM.