Ulifanya mazungumzo na Rais Kenyatta sio Raila, Elachi amsuta Kalonzo

Muhtasari

• Beatrice Elachi ametupilia mbali madai kwamba Kalonzo alifanya mazungumzo na Raila Odinga.

• Alisema kwamba Kalonzo hapaswi kulazimisha Odinga kumpa wadhfa wa mhgombea mwenza.

Katibu mkuu mwandamizi katika kitengo cha jinsia ya umma, Beatrice Elachi.
Katibu mkuu mwandamizi katika kitengo cha jinsia ya umma, Beatrice Elachi.
Image: Facebook

Aliyekuwa spika wa Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amemkashifu Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu kile alichodai kuwa alimvuta kiongozi  wa ODM Raila Odinga kwenye makubaliano ambayo hakuhusika kwayo.

Katika mahojiano na  runinga ya K24 Jumanne, Elachi alisema mazungumzo kati ya Kalonzo na Rais Uhuru Kenyatta hayakumhusisha Raila.

"Kalonzo alikaa na Rais na kujadiliana na sio na Waziri Mkuu wa zamani," Elachi alisema.

Zaidi ya hayo, alitilia shaka makubaliano kati ya Kalonzo na Rais Kenyatta.

“Kalonzo alisema hawezi kujadiliana na Raila na hivyo akafanya mazungumzo na Rais. Mkataba gani huu uliokuwa nao na Rais? Unamvuta Raila katika kitu ambacho hakuwahi kushiriki,” Elachi alisema.

Elachi alisema Kalonzo alifaa kujiunga na muungano wa Azimio la Umoja kwa mikono safi na kufanya kazi kwa ushirikiano  ili kuhakikisha Raila anakuwa rais ajaye, badala ya kung'ang'ania mdahalo wa mgombea mwenza.

Kalonzo katika siku za hivi majuzi ametangaza nia yake katika nafasi ya mgombea mwenza kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mnamo Jumatatu, Musyoka aliomba kanisa limwombee anapopigania nafasi hiyo katika Vuguvugu la Azimio la Umoja.

Kalonzo alidai baadhi ya watu wanapanga  njama usiku kucha kumfungia nje ya wadhifa huo  huku wadhifa huo unaoongozwa na Raila Odinga ukitaka kuunda serikali ijayo.

"Wanahangaika kupanga njama nani atakuwa mgombea mwenza na nani hatakuwa mgombea mwenza. Tafadhali wasaidie kubadilika na kujua kwamba alichokusudia Mungu hakuna mwanadamu atakayekizuia."

Alijiamini kuwa mapenzi ya Mungu yatatawala na atakuwa mgombea mwenza wa Raila kama ilivyokuwa 2013 na 2017.