"Digrii yangu si feki jamani" Seneta Cleophas Malala ajitetea kwa uchungu

Muhtasari

• Seneta wa Kakamega Cleophas Malala amepuuzilia mbali madai kwamba digrii yake ni bandia.

• Madai hayo yamekuwa yakienezwa na mfanyibiashara Cleophas Shimanyula.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala
Seneta wa Kakamega Cleophas Malala
Image: Screengrab:YouTube

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala amejitetea vikali dhidi ya madai kwamba shahada yake ni  bandia.

Katika mahojiano na runinga moja ya Magharibi mwa Kenya, Malala alipuuzilia mbali madai yanayomhusisha na kumiliki shahada bandia na kusema kwamba aliingia chuo cha Moi mwaka 2004 kwa mafunzo ya digirii ya uanasheria, kitivo ambacho babake hakukikubali na kupelekea kumhamisha hadi chuo cha kibinafsi cha USIU.

“Baada ya babangu kunihamisha kutoka Moi, nilikubaliwa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani (USIU) kusomea Shahada ya Sayansi katika Teknolojia ya Mifumo ya Habari. Ni wakati wa kuhitimu kwangu ambapo nilifahamisha wanafamilia yangu kuhusu nia yangu ya kujiunga na siasa,” Malala alijitetea.

Mwanasiasa huyo anayelenga kumrithi gavana Wycliffe Oparanya kama gavana wa pili wa Kakamega alisema kwamba alichukua cheti cha shahada yake kutoka USIU mwaka 2019.

Uvumi kuhusu uwezekano wa Malala kumiliki digrii bandia umekuwa ukienezwa na wapinzani wake wakiwemo mfanyabiashara Cleophas Shimanyula ambaye anamuunga mkono Ferdinand Barasa katika kinyang’anyiro hicho.

Wagombea wengine wanaowania nafasi hiyo pamoja na Malala ni mbunge wa Lugari Ayub Savula.