Kabogo afichua hamu yake wakati wa kampeni baada ya kuidhinishwa kuwania kiti cha ugavana wa Kiambu

Muhtasari
  • Kabogo afichua hamu yake wakati wa kampeni baada ya kuidhinishwa kuwania kiti cha ugavana wa Kiambu
WILLIAM KABOGO
Image: WILLIAM KABOGO/TWITTER

Aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Kiambu William Kabogo ameidhinishwa kuwania kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huu.

Kabogo kupitia kwenye mitandao yake ya kijamii alitangaza habari hiyo akisema ana hamu ya kushirikiana na wapiga kura wa Kiambu katika kipindi chote cha kampeni.

"Nimewasilisha hati zangu za uteuzi kwa Halmashauri ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya Chama cha Tujibebe. Nimeidhinishwa kugombea nafasi ya Gavana wa Kaunti ya Kiambu. Mimi hamu ya kushirikiana na watu wa Kiambu katika kipindi chote cha kampeni," alisema.

Aliongeza kuwa yuko tayari kukabiliana na wagombea wengine bila kujali itikadi za vyama vyao na atajitahidi kadri ya uwezo wake wote kuhakikisha anashinda kiti hicho.

Mwenyekiti wa NEB wa Tujibebe Lucy Kamau alisema walifanya uteuzi wao bila hitilafu au dosari zozote.

Kabogo aliipongeza bodi hiyo kwa kazi yao na kuthibitisha kuwa hakuna njia za mkato katika uhakiki.

"Ilinibidi kuleta karatasi zangu zote kwa uchunguzi," aliongeza.

Kabogo alishindwa na Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu katika uchaguzi mkuu wa 2017.