Mgombea kiti cha ugavana wa Nairobi Polycarp Igathe amefichua kuwa wagombeaji wengine wanaowania kiti hicho chini ya Azimio La Umoja Movement Coalition Party wamemwidhinisha.
Katika mahojiano yake na wanahabari Alhamisi jioni baada ya mkutano na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi, Igathe alisema kuwa sasa atapeperusha bendera ya Azimio.
"Ninafuraha sana kuwaambia kuwa tayari wamenithibitishia kuwa wataniunga mkono kama gavana wa Kaunti ya Nairobi na tunaenda pamoja kama timu," Igathe alisema.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wengine wa Azimio, akiwemo kinara wa ODM Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Martha Karua miongoni mwa wengine.
Alisema kulikuwa na makubaliano kutoka kwa mkutano huo.
Hata hivyo, Igathe alisema kuwa uthibitisho huo ni wa mdomo, na kwamba uongozi wa Azimio unatarajiwa kutangaza suala hilo leo siku ya Ijumaa.
“Katika suala la mashauriano mazungumzo ya mdomo hayathibitishwi, kinachothibitishwa ni kile kinachotoka kwa viongozi wa chama chetu lakini kwa upande wangu nataka kuwapongeza.
Aliongeza kuwa hatua ya wawaniaji wengine kuacha azma zao ili kumuunga mkono ni kuhusu ushindi wa Azimio la umoja , na si kama watu binafsi.
Igathe alieleza imani yake kwamba Azimio itatoa tangazo hilo Ijumaa, ikiwa ni pamoja na jinsi nafasi nyingine zitakavyojazwa.
Haya yanajiri huku mwaniaji wa kiti cha ugavana wa Nairobi Tim Wanyonyi akisisitiza kuwa atawania ugavana Agosti 9.