Raila aondoka nchini kwa ziara ya wiki moja Marekani

Muhtasari

•Raila pia atatumia ziara hiyo kuelezea ajenda yake na kuonyesha umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.

•Hii itakuwa safari ya mwisho ya Kimataifa ya kinara huyo wa ODM kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Image: TWITTER// RAILA ODINGA

Mgombea urais wa Muungano wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga, aliondoka nchini Ijumaa jioni kwa ziara ya wiki moja nchini Marekani.

Kinara huyo wa ODM aliondoka siku ambayo chama chake kilikuwa kinakamilisha kura za mchujo kabla ya siku ya makataa ya kuwasilisha orodha ya wagombea iliyowekwa na IEBC kufika  .

Ziara hiyo inajiri huku kukiwa na kampeni zilizonoga za  kinyang'anyiro cha kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ambaye anastaafu mwezi Agosti.

Raila anaondoka nchini wakati ambapo wakuu wa muungano wa Azimio wakianza msako wa  anayefaa kuwa mgombea mwenza wake.

Mnamo Alhamisi, Baraza la Azimio mnamo Alhamisi liliafikia kuteua jopo la ushauri ili kupendekeza wagombea wenza kwa Raila.

Hii itakuwa safari ya mwisho ya Kimataifa ya kinara huyo wa ODM kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Atatumia wiki moja huko Washington DC na San Francisco ambapo atakutana na wafanyabiashara mashuhuri na wakuu wa teknolojia.

Anatarajiwa pia kukutana na maafisa wakuu wa serikali ya Marekani, wabunge na viongozi wakuu wa Afrika waliochaguliwa.

"Atakutana na kuhutubia Wakenya walioko Marekani na kuzungumza na wataalamu kadhaa," msemaji wa Sekretarieti ya Kampeni ya Urais ya Raila Odinga, Makau Mutua alisema katika taarifa.

Raila pia atatumia ziara hiyo kuelezea ajenda yake na kuonyesha umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.

"Bw Odinga atachukua fursa ya ziara hiyo kuelezea maono yake kwa Kenya, kusisitiza umuhimu wa uhusiano wa kimkakati na wa kihistoria wa Marekani/Kenya na maslahi muhimu ambayo nchi hizo mbili zinashiriki katika eneo hili," Makau alisema.

Raila pia "atakuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji nchini Kenya katika Tehama na teknolojia na ushirika na Wakenya nje ya nchi."

Raila aliandamana na magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), James Ongwae (Kisii), Ndiritu Muriithi (Laikipia), kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Sally Kosgey.

Wengine walikuwa Seneta wa Homabay Moses Kajwang’, Mbunge wa Kathiani Robert Mbui, aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Marekani Elkanah Odembo na Mutua