Raila ndiye mgombea rais maarufu zaidi Nairobi, Mombasa, Makueni- Kura ya maoni

Muhtasari

•Raila anasalia kuwa mgombea maarufu zaidi katika Kaunti ya Nairobi kwa 41 %, Mombasa kwa  50% na Makueni kwa 48%.

•Anafuatwa kwa karibu na Naibu Rais William Ruto wa Kenya Kwanza kwa asilimia 26 jijini Nairobi na asilimia 32 mjini Mombasa. 

Kinara wa ODM Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Mgombea urais kwa tikiti ya muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga ndiye mgombea urais anayependelewa zaidi katika kaunti tatu.

Hii ni kwa mujibu wa kura ya maoni ya Trends & Insights for Africa (Tifa), ambayo ilitolewa Jumanne, Mei 3.

Kulingana na kura ya maoni ya Tifa, Raila anasalia kuwa mgombea maarufu zaidi katika Kaunti ya Nairobi kwa 41 %, Mombasa kwa  50% na Makueni kwa 48%.

Anafuatwa kwa karibu na Naibu Rais Anafuatwa kwa karibu na Naibu Rais William Ruto wa Kenya Kwanza kwa asilimia 26 jijini Nairobi na asilimia 32 mjini Mombasa. . Umaarufu wa Ruto ni 18% katika Makueni.

Ijapokuwa Raila Odinga ndiye mgombeaji urais maarufu zaidi jijini Nairobi, pengo kati yake na DP Ruto ni dogo vya kutosha kupendekeza kwamba kiwango cha ushindani katika kaunti hii kitakuwa cha juu,” Tifa alisema.

Kuna asilimia kubwa ya watu ambao hawajaamua.  Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alitajwa ingawa hajatangaza nia ya kuwania urais.

ODM ndicho chama maarufu zaidi Mombasa kwa asilimia 36 kikifuatiwa na UDA kwa asilimia 23. Asilimia 35 ya watu waliohojiwa hawakuamua.

Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya unaungwa mkono  zaidi kwa asilimia 41 ikifuatiwa na Kenya Kwanza kwa asilimia 27. Asilimia 32 bado hawajaamua.

Katika Makueni, Wiper cha Kalonzo ndicho chama maarufu zaidi kwa asilimia 43, kikifuatwa na UDA kwa asilimia 17, ODM asilimia 10 huku asilimia 25 ya waliohojiwa wakiwa hawajaamua.

Azimio la Umoja One Kenya Coalition kwa upande mwingine inaongoza kwa asilimia 62, ikifuatiwa na Kenya Kwanza kwa asilimia 13 katika kaunti hiyo.

ODM ndicho chama maarufu zaidi Nairobi  kwa asilimia 26, kikifuatwa na UDA kwa asilimia 22 huku asilimia 44 wakiwa hawajaamua.

Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ndio unaoungwa mkono zaidi kwa asilimia 42 katika kaunti ya Nairobi na Kenya Kwanza inaungwa mkono na 22% . Asilimia 36 bado hawajaamua.

Kulingana na Tifa, utafiti huo ulifanywa Aprili 2022. Wahojiwa 1,949 katika kaunti za Nairobi, Makueni na Mombasa walishiriki. Upeo wa makosa ulikuwa 4%

Madhumuni ya jumla ya utafiti huo yalikuwa kubainisha vyama na miungano maarufu ya kisiasa, wawaniaji maarufu wa nyadhifa za urais, ugavana, useneta na wawakilishi wanawake katika Nairobi, Mombasa na Makueni.