(+Video) Mwanasiasa wa UDA ajipata matatani kwa kuwatupia watu vipande vya keki 'kama kuku'

Muhtasari

•Wamuratha alirekodiwa akitupia watu  vipande vya keki kama jinsi mfugaji anavyowatupia kuku wake mahindi.

•Muratha amekosolewa sana kufuatia video hiyo huku wanamitandao wengi wakionekana kughadhabishwa na kitendo chake.

Image: FACEBOOK// ANNE MURATHA

Mpeperusha bendera ya UDA katika kinyang'anyiro cha uwakilishi wa wanawake wa Kiambu, Anne Wamuratha amejipata matatani baada ya video yake akitupia umati wa watu vipande vya keki kusambaa mitandaoni.

Katika video hiyo iliyorekodiwa katika uwanja wa Ruiru, Wamuratha anaonekena akitupia watu  vipande vya keki kama jinsi mfugaji anavyowatupia kuku wake mahindi. Watu waliokuwa wamejumuika pale wanaonekana wakiinua mikono yao juu katika juhudu za kufikia vipande vile vya keki.

Kabla ya kuanza kutupa keki ile, mtaalamu huyo wa masuala ya ndoa alisikika akiwaagiza wakazi wajipange vizuri ili kila mmoja aweze kufikiwa na kipande angalau.

Muratha amekosolewa sana kufuatia video hiyo huku wanamitandao wengi wakionekana kughadhabishwa na kitendo chake.

Video hiyo imekuwa ikivuma hasa katika mtandao wa Twitter ambako mamia ya Wakenya wamejitokeza kueleza ghadhabu yao.

Haya hapa baadhi ya maoni ya Wakenya:-

@paulinenjoroge Mgombea kiti cha mwakilishi wa wanawake wa Kiambu kwa tikiti ya UDA Wamuratha akishiriki mpango wa kupatia kuku chakula.. oops nilimaanisha kupatia mpango wa kupatiana keki.

@CaxstomePkigata Mgombea kiti cha mwakilishi wa wanawake wa Kiambu kwa tikiti ya UDA Anne Muratha anaonekana akitupa chakula kwa watu wenzake wa Kiambu katika uwanja wa Ruiru kama kwamba anapatia kuku chakula. Hii inatiua uchungu, inadhalilisha na ni kukosa utu.

@pterkarnja Mgombea kiti cha mwakilishi wa wanawake wa Kiambu kwa tikiti ya UDA Wamuratha amefanikiwa kutojipigia debe. Alikuwa anafikiria nini?? Acha aombe ushauri kwa gavana wa zamani. Atahitaji bahati kubwa.

@DrJuma_M Hiivideo ya Wamuratha inasumbua sana.

Anne Muratha alishinda tikiti ya UDA katika kura ya mchujo iliyofanyika mwezi jana. Aliwabwaga wanawake wengine wakiwemo mwanamuziki Loise Kim, mwanasaikolojia  Gladys Chania, MCA mteule Serah Kamunyi, Grace Wanjiku, Njeri Bakari, Pauline Agondoa, Juliet Wainaina na Mercy Nungari.