"Heshima si utumwa!" Ruto akashifu hatua ya Azimio kumhoji Kalonzo

Muhtasari

•Ruto amesema kumpeleka kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwenye mahojiano ya wagombea wenza  ni  kumvunjia heshima.

•Jopo linatarajiwa kuwasilisha majina mawili ambayo Raila na Rais Uhuru Kenyatta watachagua kama  mgombea mwenza  katika Azimio.

Naibu Rais William Ruto akiwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika majengo ya Bunge wakati wa kutazamwa kwa mwili wa Rais mstaafu Mwai Kibaki.
Naibu Rais William Ruto akiwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika majengo ya Bunge wakati wa kutazamwa kwa mwili wa Rais mstaafu Mwai Kibaki.
Image: DPPS

Naibu Rais William Ruto amesema kuwa kumpeleka kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwenye mahojiano ya wagombea wenza  ni  kumvunjia heshima.

Katika taarifa yake ya Jumatano, naibu rais alisisitiza kuwa kila kiongozi anastahili heshima.

Ruto aliongeza kuwa ni lazima Wakenya waungane ili kuondoa utamaduni wa uongo katika siasa, tabia  ambayo baadhi ya wanasiasa wanafahamika kuwa nayo.

"Ingawa sisi ni washindani, lakini kumuweka HE Kalonzo kwenye’ mahojiano’ ya kufedhehesha ni kutokujali. Ni lazima tuungane kuondoa utamaduni wa ghilba za kisiasa, sifa ya baadhi ya wanasiasa. Kwa vyovyote vile kila kiongozi anastahili utu na heshima. Heshima si utumwa. ," Ruto alisema.

Haya yanajiri huku kukiwa na hali ya taharuki katika kambi ya Kalonzo Musyoka ambapo baadhi ya washirika wamemtaka asijitokeze kwenye mahojiano ya mgombea mwenza wa Raila.

Wanabainisha kuwa Kalonzo amekuwa makamu wa rais kwa miaka mitano, na amewahi kumuidhinisha Raila mara mbili. Wanasisitiza kuwa kwenda kwenye mahojiano itakuwa ni kukosa heshima.

Mbunge wa Makueni Daniel Maanzo alisema bosi huyo wa Wiper lazima asifedheheshwe mbele ya jopo, akionya kuwa Raila anahatarisha  kupoteza kura za Ukambani ikiwa mtu wao hatapata tikiti.

“Chaguo ni lake (Raila). Akitaka kuwa Rais amtafute Kalonzo. Sitamshauri kiongozi wa chama changu kufika mbele ya jopo lolote la uhakiki ili kuambiwa ataje majina yake kama yanavyoonekana kwenye kitambulisho. Huo ni uchafu,” Maanzo alisema.

Mchakato wa uteuzi ulioundwa na Azimio umezua uvumi kwamba Kalonzo anaweza kuchukua jukumu tofauti.

Timu ya viongozi saba wa kidini na mwakilishi wa Kalonzo wanatarajiwa kuwasilisha majina mawili ambayo Raila na Rais Uhuru Kenyatta watachagua kama  mgombea mwenza  katika Azimio.

Kalonzo pia amepinga kwanini afanyiwe mtihani ili awe naibu wa Raila.

“Suala hili limeanza kunielemea sana. Naona haikubaliki kuijadili. …. Suala hili likitatuliwa mapema, litatupa baadhi yetu msukumo wa kufanya kampeni,” Kalonzo alisema wiki jana.

Kwa kupuuza jopo la mchujo, bosi wa Wiper anahatarisha kuachwa nje ya uteuzi wa Raila wa mgombea mwenza, jambo ambalo linaweza kuzidisha mvutano katika muungano huo.

Jopo hilo lina siku sita haswa - hadi Mei 10 - kupendekeza jina kwa Raila.

Katika ratiba zilizorekebishwa za IEBC, wanaowania urais wana hadi Mei 16 kuwasilisha majina yao pamoja na wagombea wenza wao.