Junet:Kwa nini ni lazima Azimio kumhoji mgombea mwenza wa Raila

Muhtasari
  • Mnamo Aprili 27, Raila alitangaza jopo la wanachama saba kuwachunguza wale wanaotaka kuwania nafasi ya mgombea mwenza
JUNET.jfif
JUNET.jfif

Katibu mkuu wa baraza la Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Alliance Junet Mohamed amefichua ni kwa nini muungano huo lazima umhoji mtu ambaye atakuwa naibu wa Raila Odinga kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

Katika ujumbe wake wa Twitter siku ya Jumanne, Mbunge huyo wa Suna Mashariki alisema kwamba sababu kuu ambayo itawabidi kuwachunguza watu wanaotarajiwa kuwa wagombea ni kwa sababu hawataki kuishia na mtu kama naibu rais wa sasa.

"Kanuni inayoongoza katika kutambua mgombea mwenza wa mgombea Urais wa Azimio ni kwamba, hatutaki kuwa na naibu wa rais kama William Ruto," Junet alisema.

Matamshi yake yanakuja huku kukiwa na maswali kuhusu ni kwa nini wawaniaji wenza wa Raila Odinga wanapaswa kuchunguzwa na kuhojiwa.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ni miongoni mwa walioibua hoja kuhusu uamuzi huo, akisisitiza kuwa amemteua Raila mara mbili, 2013 na 2017, na amehudumu kama Makamu wa Rais wa Kenya kwa miaka mitano.

“Suala hili limeanza kunilemea sana. Naona kama jambo lisilokubalika kulijadili... Suala hili likitatuliwa mapema, litawapa baadhi yetu msukumo wa kampeni,” Kalonzo alisema wiki jana.

Mnamo Aprili 27, Raila alitangaza jopo la wanachama saba kuwachunguza wale wanaotaka kuwania nafasi ya mgombea mwenza.

Jopo hilo linajumuisha makasisi na wawakilishi wa vyama vya siasa.