Wanasiasa wanaotaka kuwa naibu wa Raila wapewa masaa 24 kuwasilisha maombi

Muhtasari

•Kamati hiyo ilisema watamchagua naibu wa Raila kutoka vyama vinavyounda muungano wa Azimio.

Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Jopo lililotwikwa jukumu la kutafuta mgombea mwenza wa kinara wa ODM Raila Odinga limewapa wale wanaomezea mate nafasi hiyo masaa 24  kutuma maombi yao.

Jopo hilo mnamo Alhamisi lilivitaka vyama 26 vya kisiasa vya Azimio kuwasilisha majina ya wanaopendekezwa kwa timu inayoongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Kwanza, Noah Wekesa.

“Kamati inaomba wanachama wowote wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya wanaotaka kuteua mtu yeyote kwa ajili ya kuzingatiwa kama mgombeaji wa nafasi ya Naibu Rais wa muungano huu kuwasilisha majina yao kabla ya kufungwa kwa shughuli za kesho, Alhamisi. , Aprili 5, 2022," Wekesa alisema.

Kamati hiyo ilisema watamchagua naibu wa Raila kutoka vyama vinavyounda muungano wa Azimio.

"Kamati itazingatia tu wagombeaji ambao ni wanachama wa vyama vinavyounda Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya," Wekesa aliongeza.

Katika kile kinachoonekana kama kupunguzwa kwa matakwa ya awali ya kusaili wawaniaji wa nafasi hiyo, Kamati ilifafanua kuwa wagombea wanaotaka kujitokeza na kutoa mada mbele ya jopo la wajumbe ndio watakaoruhusiwa kufanya hivyo.

(Utafsiri: Samuel Maina)