'Inauma!' Mgombea wa ubunge wa Kamukunji Alinur Mohamed aeleza kusikitishwa na Azimio La Umoja

Muhtasari
  • Mohamed hata hivyo bado hajatangaza iwapo atawania kiti hicho kama mgomea huru licha ya wafuasi wake kumtaka achukue njia hiyo
ALINUR MOHAMED
Image: KWA HISANI

Mgombea wa nafasi ya ubunge wa Kamukunji Alinur Mohamed ameelezea kutoridhishwa na uamuzi wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wa kugawa kanda ya Nairobi ili kutambua maeneo ambapo vyama chini ya mwavuli wake vitasimamisha wagombea.

Kupitia kwenye ukurasa wake wa twitter Alhamisi Mohamed, ambaye alikuwa anataka kuwania kiti hicho katika uchaguzi wa Agosti kwa tikiti ya ODM, alipuuza mkakati wa kugawa maeneo na kuutaja kuwa tishio kwa demokrasia kwani wagombeaji wengi watafungiwa nje ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti kama matokeo.

Kufuatia hatua hiyo ya Azimio, mbunge wa sasa wa Kamukunji Yussuf Hassan wa Jubilee Party atatetea kiti hicho kwenye uchaguzi wa Agosti.

"Kwa bahati mbaya, Jimbo la Kamukunji limetengwa kwa ajili ya Chama cha Jubilee na kufanya watu wa Kamukunji wasiweze kupata kiongozi wanayemchagua. Hii inatia uchungu sana, hii inakatisha tamaa. na ni tishio kwa demokrasia yetu," Alinur Aliandika.

Vile vile alilalamika kwamba uwekezaji aliomwaga katika kampeni zake umeonekana kupungua, licha ya juhudi za kuuza manifesto yake kwa watu wa Kamukunji kwa miaka minne iliyopita.

"Nimefanya kampeni kwa miaka minne iliyopita, nikiuza ajenda yangu kwa wananchi na kufanya shughuli nyingi za kubadilisha maisha katika Jimbo la Kamukunji. Nimeuza mali yangu yenye thamani ya mamilioni ya shilingi na kutumia fedha hizo kufanya kampeni ili kuhakikisha ndoto yangu ya kuhudumia," alisema.

Mohamed hata hivyo bado hajatangaza iwapo atawania kiti hicho kama mgomea huru licha ya wafuasi wake kumtaka achukue njia hiyo.