Kalonzo akita kambi Pwani kumpigia debe Raila

Muhtasari

Akitangaza ratiba yake siku ya Jumatano kiongozi huyo wa Wiper alisema atatumia ziara hii kunadi sera za mgombea Urais wa Azimio One Kenya Raila Odinga.

 

KINARA WA WIPER KALONZO MUSYOKA
Image: WILFRED NYANGARESI

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amekita kambi katika maeneo kadha ya Mombasa Road hadi Pwani kumpigia debe Mgombea Urais wa Azimio-One Kenya Raila Odinga.

Kalonzo ambaye ameanza ziara yake leo Alhamisi  atakita kambo katika maeneo hayo kwa siku mbili ambapo atakutana na wananchi katika Barabara ya Mombasa kuanzia Mlolongo hadi Mtito Andei ikijumuisha kaunti nne za Machakos, Makueni, Kajiado na Taita Taveta.

Siku ya pili, Kiongozi huyo wa Wiper anatarajiwa kuzuru Voi, MacKinnon hadi Mombasa ambapo atafanya mikutano kadhaa ya hadhara mjini Mombasa.

Kalonzo ataandamana na mgombea Ugavana wa Machakos kwa tiketi ya Wiper Wavinya Ndeti, Mbunge Patrick Makau wa eneo bunge la Mlolongo, Mwaniaji wa Ugavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jrn, Mwakilishi wa kike Rose Museo na Mgombea wa Useneta Daniel Maanzo.

Akitangaza ratiba yake siku ya Jumatano kiongozi huyo wa Wiper alisema atatumia ziara hii kunadi sera za mgombea Urais wa Azimio One Kenya Raila Odinga.

Alisema wakati huu lazima wabadili mbinu za kufanya kampeini  “ikiwa tu tunatazamia ushindi mkubwa".