Baadhi ya wanasiasa kutumia pesa za 'Wash Wash' kunua nyadhifa - Matiang'i

Muhtasari

•  "Tunaweza kuwa na zaidi ya 40% ya waliochaguliwa kuwa viongozi wetu ikiwa tutaruhusu magenge yote ya 'wash wash' na wahalifu wengine kuhonga njia zao katika chaguzi zijazo," alisema. 

• Alihusisha hili na ulegevu wa kanuni za kifedha ambazo zinawafanya wanasiasa kuvuruga mchakato wa uchaguzi kwa manufaa yao ya kibinafsi. 

Waziri wa usalama Fred Matiang'i
Image: FRED MATIANG'I/TWITTER

Wizara ya Mambo ya Ndani imeelezea wasiwasi wake kuwa huenda baadhi ya wanasiasa watatumia pesa ‘haramu’ kununua nafasi zao bungeni na nyadhifa zingine za kisiasa. 

Kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i, kulikuwa na hofu kwamba huenda zaidi ya asilimia 40 ya watakao chaguliwa kwa nyadhifa mbali mbali watatumia pesa zilizopatikana kwa njia haramu kutokana na ufujaji wa pesa ili kuchaguliwa. 

Alihusisha hili na ulegevu wa kanuni za kifedha ambazo zinawafanya wanasiasa kuvuruga mchakato wa uchaguzi kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Bunge lilifanyia marekebisho Sheria ya Uchaguzi na kufuta vipengele vilivyokuwa vikitaka kuweka ukomo wa fedha zinazoweza kutumiwa na vyama vya siasa na wagombea wakati wa kampeni. 

Akizungumza wakati wa Kongamano la Kitaifa la kila mwaka kuhusu mageuzi ya haki ya jinai katika eneo la Naivasha, Matiang’I alitaja hali hiyo kuwa ya wasiwasi.

Akiwahutubia washiriki, Waziri huyo alionya kuwepo uwezekano mkubwa kwa wahalifu kununua njia zao ili kuingia ofisini kupitia pesa za ‘wash wash’ .

 "Tunaweza kuwa na zaidi ya asilimia 40 ya waliochaguliwa kuwa viongozi wetu ikiwa tutaruhusu magenge yote ya 'wash wash' na wahalifu wengine kuhonga njia zao katika chaguzi zijazo," alisema. 

Hata hivyo aliiondolea IEBC kuhusiana na mfumo dhaifu wa udhibiti wa ufadhili wa kampeni akisema kuwa mfumo wa kisheria wenye masharti magumu utahitaji mkabala wa sekta mbalimbali.

Wakati wa mkutano wa Naivasha, Waziri pia alitaja matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kama chanzo kingine cha wasiwasi kuhusu usalama na uaminifu wa uchaguzi.

"Tuna changamoto ya dhamana nyingi zinazotolewa na mahakama zetu na baadhi ya watu ambao wamekamatwa wanafurahia dhamana yao ya nane, tisa au kumi," alisema.

Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i akizungumza na Jaji Mkuu Martha Koome (kushoto) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji wakati wa Kongamano la Kitaifa la kila mwaka la mageuzi ya haki ya jinai, Naivasha mnamo 10/5/22.
Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i akizungumza na Jaji Mkuu Martha Koome (kushoto) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji wakati wa Kongamano la Kitaifa la kila mwaka la mageuzi ya haki ya jinai, Naivasha mnamo 10/5/22.
Image: Antony Gitonga

Ili kufanikisha uchaguzi mkuu, CS alisema angalau maafisa 10,000 maalumu wamehamasishwa na kutumwa chini ya mkabala wa sekta mbalimbali.

"Serikali pia ingeshirikiana kwa karibu na IEBC na washikadau wengine ili kuhakikisha uchaguzi huo ulifanywa kwa njia ya kuaminika," akasema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amewahakikishia wakenya uchaguzi huru na wa haki akiongeza kuwa tume hiyo imepanga kufanya uchaguzi wa tarehe 9 Agosti.

  Aliongeza kuwa katika siku chache zijazo, watakabidhi orodha ya wawaniaji kwa EACC na mashirika mengine muhimu ya serikali kwa uchunguzi zaidi.

"Tulijifunza vyema mwaka wa 2017 na sote tumejitayarisha kufanya uchaguzi wa kuaminika usio na vurugu na utashi wa watu kuwakilishwa," alisema.

Chebukati aliongeza kuwa suala tata la theluthi-mbili litabainishwa wiki zijazo wakati tume hiyo itapitia orodha ya majina yote yaliyowasilishwa na vyama vya kisiasa.