Gavana Amason Kingi na chama chake cha PAA ahamia Kenya Kwanza

Muhtasari

• Baadhi ya sababu alizotaja ni kutofanikishwa kwa utaratibu wa kisheria kwa chama cha PAA kujiunga na muungano wa Azimio rasmi.

• Kingi pia alidai kwamba kuna usiri mkubwa katika oparesheni za muungano wa Azimio akisema kwamba hakuna uazi katika mikakati ya muungano huo.

Gavana wa Kilifi Amason Kingi
Gavana wa Kilifi Amason Kingi
Image: /twitter.com/governorkingi/status

Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kimejiondoa kutoka muungano wa Azimio – One Kenya na kujiunga rasmi na muungano wa Kenya Kwanza.

Kinara wa chama cha PAA gavana wa Kilifi Amason Kingi akizungumza katika makaazi ya naibu rais mtaani Karen siku ya Jumanne alisema kwamba walilazimika kujiondoa kutoka muungano wa Azimio One Kenya kwa sababu mbali mbali.

Baadhi ya sababu alizotaja ni kutofanikishwa kwa utaratibu wa kisheria kwa chama cha PAA kujiunga na muungano wa Azimio rasmi.

Kingi pia alidai kwamba kuna usiri mkubwa katika oparesheni za muungano wa Azimio akisema kwamba hakuna uazi katika mikakati ya muungano huo.

Kulingana na sababu hizo Kingi alisema ilikuwa vigumu kwao kuendelea kushirikiana na muungano huo ili kuafikia agenda za chama hicho ambazo ni kupigania maslahi ya Wapwani.

Kingi pia alidai kwamba katika muungano wa Azimio – On Kenya hakuna agenda madhubuti inaoyolenga kuimarisha hali ya maisha ya watu wa pwani ili kuchochea maendelo katika kanda hiyo.

Gavana huyo wa Kilifi anayeondoka alisema kwamba baada ya mashauriano mafupi na ya kina na muungano wa Kenya Kwanza waliafikiana kushughulikia matakwa ya Wapwani punde tu serikali ya Kenya Kwanza itakapoundwa.

Miongoni mwa mambo mengine, Kingi alisema kwamba naibu rais William Ruto aliahidi kurejesha shughuli za baharini kutoka Naivasha hadi Pwani kama ilivyokuwa hapo awali.

Tangazo hilo la Kingi linajiri siku moja tu baada ya chama cha Maenedeleo Chap Chap kuhama muungano wa Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza.