Gavana Kivutha Kibwana azungumzia madai ya kukutana na DP Ruto

Muhtasari

•Kivutha ameeleza kuwa picha hiyo ilipigwa takriban mwaka mmoja uliopita baada ya mkutano wa baraza la magavana.

•Gavana Kibwana alimshtumu kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa kuwa kikwazo cha urais wa Raila Odinga.

Kivutha Kibwana na naibu rais William Ruto
Kivutha Kibwana na naibu rais William Ruto
Image: HISANI

Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana amelazimika kujitokeza kufafanua kuhusu picha yake na naibu rais William Ruto ambayo imekuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamiii.

Picha inayomuonyesha gavana huyo wa muhula wa pili akisalimiana na Ruto imekuwa ikivuma hasa kwenye Twitter ikidaiwa kuwa wawili hao walishiriki mkutano hivi majuzi.

Kivutha hata hivyo ameeleza kuwa picha hiyo ilipigwa takriban mwaka mmoja uliopita baada ya mkutano wa baraza la magavana.

"Nimeambiwa kuwa picha hii inavuma tena. ilikuwa picha nzuri ambayo ilipigwa baada ya mkutano wa IBEC wa baraza la magavana kati ya wengine, naibu rais wa Kenya na ilipigwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita," Kivutha alisema kupitia Twitter.

Kibwana hata hivyo alidokeza kuwa anashikilia msimamo sawa na mgombea urais huyo katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

"Aliniambia kuwa anaamini katika uchumi wa Bottom Up na nikajibu kuwa kila siku nasimama na Wanjiku," Aliendelea.

Kumekuwa na tetesi kuwa huenda Kibwana ni miongoni mwa wanasiasa wakuu wanaotarajiwa kugura  Azimio la Umoja baada ya Alfred Mutua wa Maendeleo Chap Chap kudokeza kuwa kuna baadhi ya vyama vinavyokusudia kujiondoa kwenye muungano huo.

Siku ya Jumatatu gavana huyo wa Machakos alitangaza kujiunga kwake na muungano wa Kenya Kwanza baada ya kugura Azimio.

"Naibu Rais William Ruto ni mtu mzuri na ataibadilisha nchi hii. Jana usiku (Jumapili) tulitia saini mkataba na Kenya Kwanza na nakala hii hapa," Mutua alitangaza.

Mutua alilalamikia ukosefu wa uwazi na udhalilishaji katika muungano wa Azimio unaoongozwa na rais Kenyatta na Raila Odinga.

Awali siku ya Jumatatu Kibwana alimshtumu kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka  kwa kuwa kikwazo cha urais wa Raila Odinga.

Kibwana alisema chama cha Wiper kinadhoofisha muungano wa Azimio na kuwataka rais Kenyatta na Raila kuuokoa mungano huo kabla haujazama.