IEBC yaongeza muda wa vyama kutimiza hitaji la uswa wa jinsia katika uteuzi

Muhtasari

• Kulingana na IEBC vyama vyote vya kisiasa vinahitajika kuwasilisha orodha mpya za uteuzi kufikia Alhamisi saa kumi na moja jioni.

IEBC/Twitter
IEBC/Twitter
Image: Wafula Chebukati

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imeongeza muda wa vyama vya kisiasa kutimiza hitaji la usawa wa jinsia katika orodha zao za uteuzi.

Katika taarifa siku ya Jumatatu usiku IEBC iliongeza muda huo hadi tarehe 12 Mei, 2022.

Mwenyekiti Wafula chebukati alisema kwamba muda huo ambao ulikuwa ukamilike Mei tisa hautaongezwa tena.

Chebukati hata hivyo alisema kufikia siku ya Jumatatu vyama vingi vya kisiasa vilikuwa tayari vimeafikia hitaji hilo muhimu la katiba.

Alisema kama tume waliamua kuongeza muda huo kwa sababu baadhi ya vyama vilikuwa havijatimiza hitaji la usawa wa jinsia katika orodha zao za uteuzi kutokana na muda mfupi uliokuwa umetolewa.

Kulingana na IEBC vyama vyote vya kisiasa vinahitajika kuwasilisha orodha mpya za uteuzi kufikia Alhamisi saa kumi na moja jioni.

Katiba inalazimisha kuwepo kwa angalau thuluthi moja ya jinsia moja katika nyadhifa za uwakilishi.