Kalonzo abadili msimamo na kufika mbele ya jopo la kutafuta mgombea mwenza wa Raila

Muhtasari

• Msimamo huu mpya wa Kalonzo unajiri siku moja tu baada ya mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi kujiondoa kwenye mahojiano na kutangaza kumuunga mkono kinara huyo wa Wiper.

Katibu wa jopo la mgombea mwenza wa Azimio Elizabeth Meyo, kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na Wakili Paul Mwangi wakimsindikiza Kalonzo kufika mbele ya jopo katika hoteli ya Serena mnamo Mei 10,2022.Picha/Enos Teche.
Katibu wa jopo la mgombea mwenza wa Azimio Elizabeth Meyo, kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na Wakili Paul Mwangi wakimsindikiza Kalonzo kufika mbele ya jopo katika hoteli ya Serena mnamo Mei 10,2022.Picha/Enos Teche.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amebadili msimamo wake wa awali na kufika mbele ya jopo la kuwahoji wanaotaka nafasi ya mgombea mwenza wa Raila Odinga katika muungano wa chama cha Azimio – one Kenya.

Makamu huyo wa rais wa zamani siku ya Jumanne aliweka kando vitisho vyake vya awali kuwa hawezi kufika mbele ya jopo hilo na kuwasili katika Hoteli ya Serena mwendo wa saa tatu asubuhi.

Aliingizwa katika chumba cha mahojiano na Katibu wa jopo hilo Elizabeth Meyo na mshauri wa kisheria wa Kamati hiyo Paul Mwangi.

Msimamo huu mpya wa Kalonzo unajiri siku moja tu baada ya mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi kujiondoa kwenye mahojiano na kutangaza kumuunga mkono kinara huyo wa Wiper.

Maswali ambayo jopo hilo linauliza ni pamoja na; uzoefu wa kisiasa wa mtu, sifa za kitaaluma na maswali ya jumla kuhusu jinsi ya kukabiliana na changamoto za kitaifa kama vile rushwa na ukosefu wa ajira kwa vijana.