Ruto kufufua BBI kupitia mlango wa nyuma, Azimio one Kenya yasema

Kutoka kushoto Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua katika mkutano wa hadhara 5/5/2022.
Kutoka kushoto Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua katika mkutano wa hadhara 5/5/2022.

Chama cha muungano wa Azimio –One Kenya kimemkashifu vikali naibu rais William Ruto kwa kuwahadaa wakenya kuukataa mchakato wa BBI.

Katibu mkuu wa chama cha Azimio –One Kenya Junet Mohamed siku ya Alhamisi alisema kwamba ufichuzi wa makubaliano yaliotiwa saini kuhusu vile viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza watagawana nafasi za uongozi ikiwa watashinda kura umeonyesha kiwango cha utapeli wa kisiasa katika uongozi wa Ruto.

Kulingana na Junet Ruto alikuwa akipinga vikali mchakato wa BBI akisema kwamba hauna manufaa kwa wakenya bali unalenga tu kugawa mamlaka kwa viongozi wachache.

“Amekuwa akifanya kampeni kwa misingi kwamba uongozi wake sio wa kugawa mamlaka bali unalenga maslahi ya wakenya,” Junet alisema.

Kulingana na ufichuzi kuhusu makubaliano yaliotiwa saini na viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza:

 chama cha UDA chake naibu rais William Ruto kitapewa nafasi ya Urais na Naibu rais, kinara wa ANC Musalia Mudavadi atatengewa nafasi ya waziri mkuu, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula atapata nafasi ya Spika wa bunge la Kitaifa, kiongozi wa chama cha PAA Amason Kingi atakabidhiwa nafasi ya spika wa seneti huku gavana wa Machakos ambaye pia ni kinara wa Maendeleo Chap Chap Alfred Mutua akipewa nafasi ya uaziri.

Junet ambaye alikuwa ameandamana na gavana Hassan Joho mjini Malindi walieleza kutamaushwa kwao na hatua ya UDA kupanga ugavi wa nafasi za uongozi kama vile ya waziri mkuu, jambo walilolipinga wakati wa mchakato wa BBI. 

Walitaja hatua hii kama siasa ya utapeli.

 “UDA Ni matapeli wasiofaa kuongoza taifa, walipinga mikakati ya kugawa nafasi za uongozi kama ilivyopendekezwa awali kwenye BBI, sasa wao wanagawanya mamlaka,”  Junet alisema.

Joho alisema kwamba baadhi ya nafasi za kiasiasa zilizobuniwa na Kenya Kwanza katu hazitaleta suluhu kwa changamoto zinazomkumba mkenya wa kawaida na hasa kanda ya Pwani. 

‘Bandari ya Mombasa isitumiwe kisiasa , tumesema tutajadili na kufikiria upya kuhusu majukuku na utendakazi wa bandari”, Joho alisema.

Akizungumzia usemi wa gavana wa Kilifi Amazon Kingi Joho alisema… “Huwezi kutatua shida za watu wetu kwa nafasi ya kibinafsi. Wewe ukiwa spika utaajiri watu wangapi wa pwani, ukiwa spika utabadilishaje utendakazi wa bandari”.

Junet alisema kwamba ni wazi kuwa viongozi Musalia Mudavadi, Moses Wetangula, Amason Kingi na Afred Mutua na wakenya kwa jumla wamelaghaiwa na naibu rais.

Gavana Joho alishangaa vile Mudavadi na Wetangula wataweza kumletea ruto asilimia 70  ya kura za magharibi mwa Kenya, akisema kwamba hiyo ni njia moja ya kuwatema viongozi hao.

“Tumegundua kwamba bodaboda na mama mboga ambao Ruto amekuwa akiwaambia wakenya ni Mudavadi, Wetangula, Kingi na Mutua,” Joho alisema.

Kulingana na Joho alitarajia kuona wakenya wa kawaida katika orodha ya ugavi wa nafasi katika muungano wa Kenya Kwanza kama alivyokuwa akisema naibu rais.

Junet alikashifu naibu rais William Ruto kwa kuidhalilisha hadhi ya Mudavadi na kumfanya kama mtumwa kwa kumtaka amletee kwanza asilimia 70 ya kura za magharibi kabla ya kupewa nafasi yoyote ile.

“Kumlazimisha Mutua kuleta asilimia 35 ya kura za ukambani kabla umpe kitu ni utapelin wa hadhi ya juu”, Junet aliongeza.