Andrew Sunkuli: Mfahamu mgombea mwenza wa Kalonzo Musyoka

Muhtasari

•Kabla ya kuteuliwa katika nafasi ya mgombea mwenza wa Kalonzo, Sunkuli alikuwa ameteuliwa kuwania useneta wa Narok kwa tikiti ya Wiper.

•Kando na ualimu, Sunkuli pia ni mwandishi, mfanyibiashara, mfanyakazi wa jamii na mwanasiasa.

Kalonzo Musyoka amemtueua Andrew Senkuli kuwa mgombea mwenza wake
Kalonzo Musyoka amemtueua Andrew Senkuli kuwa mgombea mwenza wake
Image: WILFRED NYANGARESI

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ametangaza kuwa atakuwa kwenye  kinyang'anyiro cha Urais cha Agosti 9.

Kalonzo amesema atapeperusha bendera ya muungano wa OKA katika kinyanganyiro hicho kuku akimteua Andrew Sunkuli kama mgombea mwenza wake.

Sio mengi yalikuwa yakijulikana kumhusu Bw Sunkuli kabla ya leo.

Kabla ya kuteuliwa katika nafasi ya mgombea mwenza wa Kalonzo, Sunkuli alikuwa ameteuliwa kuwania useneta wa Narok kwa tikiti ya Wiper.

Sunkuli ni mwalimu kitaaluma. Alihudhuria Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya mwaka wa 1985- 1988 ambapo alipata Shahada ya Elimu katika Kiingereza na Fasihi.

Mwaka wa 1988 aliajiriwa na TSC kufunza somo la Kizungu na Fasihi katika shule ya upili ya Kabarak.

Kando na ualimu, Sunkuli pia ni mwandishi, mfanyibiashara, mfanyakazi wa jamii na mwanasiasa.

Sunkuli tayari amekubali ofa ya Kalonzo ya kuwa mgombea mwenza wake huku ikiwa imesalia masaa machache tu kabla ya makataa ya kuwasilisha majina ya wagombea wenza.

""Kwa unyenyekevu wote, kwa hivyo, ninakubali uteuzi wa kuwa mgombea mwenza wa Wiper Democratic Movement," Sunkuli alisema. 

Mwanasiasa huyo alisema hakuamini wakati alipopigiwa simu na chama cha Wiper wakimuomba kuwa mwenza wa Kalonzo.

“Nilidhani tutakuwa tunakimbia pamoja kwa sababu huwa nakimbia asubuhi na wenzangu,” amesema

"Niliacha mifugo wangu bila wa kuwaangalia, wapiga kura wangu wa kaunti yangu bila wa kuwashughulikia. Sijafanya mawasiliano yoyote rasmi kwa timu yangu ya kampeni kuwa niko hapa."