Ngilu amsuta Kalonzo na kumtaka kurejea Azimio, ashutumu washauri wake

Muhtasari

• "Kalonzo kuondoka Azimio ni ubinafsi sana ya kuangazia tu uongozi kwa maana jamii ya Wakamba imekuwa nje ya serikali ya kitaifa kwa miaka 10 iliyopita," Ngilu alisema. 

 

Gavana wa Kitui Charity Ngilu
Image: Musembi Nzengu

Gavana wa Kaunti ya Kitui Charity Ngilu amemtahadharisha kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka dhidi ya kukataa wadhifa na mambo mengine aliyoahidiwa katika muungano wa Azimio. 

Mgombea urais wa Azimio, Raila Odinga, akimtambulisha Martha Karua kama mgombea mwenza wake, alitangaza kuwa Kalonzo atakuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri iwapo Azimio itaunda serikali ijayo. 

Akizungumza katika mahojiano kwenye runinga ya KTN News siku ya Jumanne, Ngilu alisema kuwa Kalonzo ni kiongozi mbinafsi na akamtaka kuweka maslahi ya watu wa Ukambani mbele. 

"Kalonzo kuondoka Azimio ni ubinafsi sana ya kuangazia tu uongozi kwa maana jamii ya Wakamba imekuwa nje ya serikali ya kitaifa kwa miaka 10 iliyopita," Ngilu alisema. 

Ngilu alisema kuwa Kalonzo hawezi kushinda uchaguzi wa Agosti peke yake. "Kuna viongozi wachache ndani ya chama cha Wiper ambao wanajua wakigombea wenyewe hawawezi kushinda uchaguzi. Lakini wanamshikilia ili wachaguliwe tena," Ngilu alisema. 

Pia aliwataja viongozi wanaomshauri Kalonzo kuwania urais kama wabinafsi. "Wanajua vyema kwamba hawezi kushinda na kuwa rais wa Kenya," alisema. 

Alisema hayo siku chache tu baada ya Kalonzo kutangaza kuwa amejiondoa katika Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na atawania urais kwa tiketi ya Wiper. 

Kinara huyo wa Wiper alisema jina lake tayari limewasilishwa kwa IEBC kama mgombeaji wa Urais wa chama hicho. 

Ngilu alishauri jamii ya Wakamba kuungana na Raila na kuwataka Wakamba kumuunga mkono Raila. 

"Sisi kama jamii ya Kamba, ikiwa hatuungi mkono Azimio, tutapoteza. Na hatuwezi kumudu kupoteza, "alisema.