Raila ampiku Ruto kwa umaarufu- Kura ya maoni

Muhtasari

•Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya wa Raila pia una umaarufu zaidi wa asilimia 38 huku asilimia 28 wakipendelea muungano wa  Kenya Kwanza.

•Tikiti ya Raila Odinga - Martha Karua imekadiriwa kuwa maarufu zaidi ikilinganishwa na ya Ruto huku 2% wakisema wangepigia kura timu ya Kalonzo Musyoka - Andrew Sunkuli.

Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga
Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga
Image: STAR

Kinara wa ODM Raila Odinga sasa anaongoza kinyang'anyiro cha urais kwa asilimia 39 akifuatiwa kwa karibu na William Ruto kwa asilimia 35, utafiti mpya wa Tifa umefichua.

Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya wa Raila pia una umaarufu zaidi wa asilimia 38 huku asilimia 28 wakipendelea muungano wa  Kenya Kwanza katika kura ambapo OKA ilipata uungwaji mkono wa asilimia 3.

Tikiti ya Raila Odinga - Martha Karua imekadiriwa kuwa maarufu zaidi ikilinganishwa na ya Ruto huku asilimia mbili pekee wakisema wangepigia kura timu ya Kalonzo Musyoka - Andrew Sunkuli.

Kati ya wahojiwa 1,719 waliohojiwa na Tifa, asilimia 14 walisema hawajaamua ni timu gani wangepigia kura huku asilimia 8 wakikosa kutoa majibu katika uchunguzi uliofanyika Mei 17.

Kulingana na kura hiyo  ya maoni, timu ya Raila ndiyo inayopendwa zaidi Nyanza kwa asilimia 69 huku timu ya Ruto ikiwa maarufu katika Bonde la Ufa Kusini na asilimia 46 katika Mlima Kenya ambapo umaarufu wa Raila ulikadiriwa kuwa asilimia 24.

Kalonzo alichaguliwa kwa asilimia 15 katika Mashariki ya Chini huku Raila na Martha wakiwa na asilimia 36 katika eneo la Ukambani akifuatwa na Ruto kwa asilimia 23.

Azimio ni maarufu zaidi katika mikoa mitano ambayo ni Pwani, Mashariki ya Chini, Nairobi, Nyanza, naRuto ni maarufu zaidi katika Ufa wa Kati, Mlima Kenya, Ufa Kusini, na Kaskazini Mashariki.