Vyama zaidi vinaelekea kuondoka Azimio- Ruto

Muhtasari

•Ruto alisema vyama hivyo vinapanga kugura muungano wa Azimio la Umoja ili kujiunga na  muungano wake.

•Ruto aliikashifu timu ya Raila akisema haina masilahi ya wananchi moyoni bali ni wanaangazia vyeo tu serikalini.

DP Ruto katika mazishi ya nduguye Rigathi Gachagua
DP Ruto katika mazishi ya nduguye Rigathi Gachagua
Image: FACEBOOK

Naibu Rais William Ruto amefichua kuwa vyama vingi vya kisiasa vimeonyesha nia ya kujiunga na vuguvugu la Kenya Kwanza.

Alisema vyama hivyo vinapanga kugura muungano wa Azimio la Umoja ili kujiunga na  muungano wake.

Ruto ambaye alikuwa akizungumza katika kaunti ya Nyeri wakati wa mazishi ya marehemu James Rerian, kakake mgombea mwenza wake  na Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, alisema viongozi wengi wameanza kuona tofauti kati ya timu yake na ile inayoongozwa na Raila Odinga.

Alitaja masaibu ambayo kiongozi wa PAA Amason Kingi na Alfred Mutua wa MCC walipitia kutafuta makubaliano ya muungano kabla ya kuondoka kwao kuwa miongoni mwa masuala yanayowashinikiza viongozi kutoka katika kambi hiyo.

"Timu hii unayoiona  nami ni kubwa na ya kutisha… Kuna wengine zaidi wanakuja kuungana nasi kwa sababu wamegundua kile tulichogundua zamani ni cha kweli," alisema.

Alitaja tukio la Jumatatu ambapo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka aliondoka Azimio baada ya kuhisi kama kwamba alichengwa  kama mojawapo ya sababu kwa nini vyama vinapanga kujiondoa Azimio.

"Haiwezekani kujadili umoja wa taifa pamoja na udanganyifu na ujanja katika uongozi wetu. Udanganyifu katika siasa zetu unadhoofisha umoja wa taifa letu, na ndiyo maana Agosti 9, wananchi wanapaswa kukataa udanganyifu ili tuwe huru na tuipeleke nchi yetu mbele,” alisema.

Vile vile aliikashifu timu ya Raila akisema haina masilahi ya wananchi moyoni bali ni wanaangazia vyeo tu serikalini.

Akirejelea dhamira yake ya kuinua viwango vya kiamisha na kuboresha uchumi wa nchi mara tu atakapochaguliwa, DP alisema Kenya Kwanza inalenga kutoacha yeyote nyuma.

Pia alimsifu  mgombea mwenza wake Gachagua akisema alikuwa mtu mwenye haiba shupavu.

"Nilikuwa nikitafuta mtu mwenye nguvu sana kwa sababu masuala ya Kenya yanahitaji wanaume na wanawake wasiobadilika-badilika, watu ambao hawawezi kuepuka wajibu au kukimbia changamoto. Wale wanaosimama na kutatua tatizo,” alisema Ruto.

Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, Moses Wetang'ula (Ford K), Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, William Kabogo, na Seneta Kipchumba Murkomen, miongoni mwa wengine walihudhuria.

Gachagua, kwa upande wake, aliapa kuwa ataendelea kuwa mwaminifu kwa Ruto iwapo watapanda mamlakani.

Mudavadi alisema, "Tunataka serikali iliyoandaliwa, inayoheshimu sheria, inayoheshimu dini na matakwa ya watu, na hiyo inapatikana Kenya Kwanza,"

Wetang'ula alisema kuwa kama timu, wamejitayarisha na kuzingatia siku zijazo, juu ya ufufuaji wa uchumi na hawatakengeushwa na kuchukuliwa mateka na "mabaki ya siku zijazo".

Kahiga alisema, "Tuna vita vikali mbele yetu."

(UTAFSIRI: SAMUEL MAINA)