KANU iko imara katika Azimio, hakuna kurudi nyuma! - Gideon Moi

Muhtasari

•Moi alisema kuwa chama chake kimedhamiria kuleta kila mtu pamoja  ili kuhakikisha mwaniaji wao wa urais Raila Odinga anakuwa rais wa tano wa Kenya.

•Moi na Kalonzo walishiriki mazungumzo jijini Nairobi siku ya Jumapili ingawa maelezo ya mkutano huo yalisalia kuwa machache.  

Kinara Raila Odinga na Seneta Gideon Moi
Image: Twitter/Gideon Moi

Chama cha Kenya African National Union (KANU)  kipo imara katika muungano wa Azimio La Umoja, kiongozi wa chama Gideon Moi amesema.

 Katika taarifa yake ya Alhamisi, Moi alisema kuwa chama chake kimedhamiria kuleta kila mtu pamoja  ili kuhakikisha mwaniaji wao wa urais Raila Odinga anakuwa rais wa tano wa Kenya.

 "KANU iko imara Azimio na hakuna kurudi nyuma. Tumedhamiria kuleta kila mtu kwenye bodi ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa  Raila kwa kuwa tunaamini katika ushirikishwaji, uhuru wa mtu binafsi na umoja wa kitaifa," alisema kwenye Twitter. 

Kupitia matamshi hayo Moi amepuuzilia mbali uvumi kwamba Kanu pia inaweza kujiondoa kwenye muungano huo baada ya Wiper ya Kalonzo Musyoka kugura.

Mnamo Jumatatu, Moi alihudhuria hafla ya Raila kwa muda, kabla ya kuondoka na kuelekea hadi katika afisi za SKM mtaani Karen ambapo Kalonzo alitangaza kuondoka Azimio na vile vile kutangaza  azma yake ya kuwania urais. 

Moi na Kalonzo walishiriki mazungumzo jijini Nairobi siku ya Jumapili ingawa maelezo ya mkutano huo yalisalia kuwa machache.  

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat alipokuwa akizungumza Jumatatu baada ya Raila kumtambulisha Martha Karua kama mgombea mwenza wake katika ukumbi wa KICC alisema chama hicho hakina mpango wowote wa kujiondoa kwenye muunganowa Azimio  ili kuungana na miungano  mingine au kuendeleza azma nyingine.

"Ninataka kumhakikishia rais wa tano wa jamhuri ya Kenya kwamba wakati huu, hesabu Kanu katika muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya. Tuko hapa kukaa na tutawapigania kwa sababu hii ndiyo timu inayoshinda,” alisema.