Gachagua adai nusu ya serikali ya Ruto

Muhtasari

•Gachagua aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kuwekeza kura zao kwa Ruto ili waweze kutuzwa kwa sehemu kubwa ya serikali.

•Gachagua pia alimtaka Ruto kujenga shule za bweni zitakazotosheleza mahitaji ya maafisa wa polisi nchini.

Mbunge Rigathi Gachagua na DP William Ruto
Image: Andrew Kasuku

Mgombea mwenza wa urais katika Kenya Kwanza Rigathi Gachagua amemtaka naibu rais William Ruto kutengea eneo la Mlima Kenya 50% ya serikali endapo atashinda urais.

Akizungumza mjini Embu siku ya Ijumaa wakati wa kongamano la kiuchumi la kaunti hiyo, Gachagua aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kuwekeza kura zao kwa Ruto ili waweze kutuzwa kwa sehemu kubwa ya serikali.

"Ninapendekeza  ombi la ugawaji wa asilimia 50 ya serikali ya Ruto," Gachagua alisema.

"Lakini kuomba hisa za serikali ni jambo moja na kupata hisa ni jambo jingine. Ili tupate sehemu kubwa, ni lazima tupige kura kwa wingi."

Mbunge huyo wa Mathira alisema kwa kuwa kiongozi wa Chama cha ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula walituma maombi ya kugawiwa asilimia 30 ya hisa na wanajitahidi kufanikisha hilo, eneo la Mlima Kenya linafaa kutoa kura nyingi ili kuongeza mgao wao.

"Umiliki wetu wa serikali hii ijayo utabainishwa na idadi ya kura tulizopiga kumuunga mkono Ruto. Kwa hivyo, tuhakikishe tunajitokeza kwa wingi na kumpigia kura Ruto," Gachagua aliongeza.

Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula walitia saini kuwasilisha asilimia 70 ya kura za Magharibi ili kupata asilimia 30 ya mgao wa serikali ya Kenya Kwanza.

Kando na hayo, Mudavadi atateuliwa kuwa katibu mkuu wa baraza la mawaziri huku Wetangula akiwa spika wa Bunge la Kitaifa.

Gachagua pia alitumia fursa hiyo kutetea mahitaji ya maafisa wa polisi nchini.

Alimtaka Ruto kujenga shule za bweni zitakazotosheleza mahitaji ya maafisa wa polisi nchini.

Alifafanua kuwa kupelekwa kwa maafisa katika maeneo mbalimbali kunatatiza masomo ya watoto wao.

"Wameomba hili kwa moyo wa Bottoms up kwa vile shule za bweni zilizopo pekee ni za watoto wa maafisa wa ngazi za juu," aliongeza.