Ruto aidhinisha MCA kuwania ubunge wa Mathira baada ya kumteua Gachagua kama mgombea mwenza

Muhtasari

•Ruto alisema MCA huyo na uwezo wa kutoshea viatu vya mbunge wa sasa wa eneo hilo Rigathi Gachagua.

•Alisema Wamumbu alionyesha ujasiri wake kwa kupinga BBI na suala la kulazimishwa kwa wabunge wa kaunti kupitisha mswada huo.

Naibu Rais William Ruto akiwa na Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua wakati wa mkutano wa hadhara huko Githunguri, Kiambu Ijumaa, Februari 18, 2022.
Naibu Rais William Ruto akiwa na Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua wakati wa mkutano wa hadhara huko Githunguri, Kiambu Ijumaa, Februari 18, 2022.
Image: Picha: DPPS

Naibu Rais William Ruto amemtambulisha MCA wa wadi ya Konyu Eric Mwangi Wamumbu kama chaguo lake la mgombea ubunge wa Mathira.

Ruto alimuidhinisha Wamumbu siku ya Jumamosi wakati wa mkutano wa Kenya Kwanza katika Mji wa Karatina, kaunti ya Nyeri.

Naibu rais alisema MCA huyo na uwezo wa kutoshea viatu vya mbunge wa sasa wa eneo hilo Rigathi Gachagua.

Gachagua anajiondoa katika kinyang'anyiro hicho kufuatia kuteuliwa kwake kuwa mgombea mwenza wa Ruto.

DP alisema Wamumbu alionyesha ujasiri wake kwa kupinga BBI na suala la kulazimishwa kwa wabunge wa kaunti kupitisha mswada huo.

"Kwa vile Gachagua anaenda Nairobi, tuko na kijana hapa ambaye anatosha kuchukua hiyo kazi. Huyu ni kijana shujaa. Ni baathi ya MCA wachache ambao walikataa pesa na wakasema hawawezi kukubali BBI. Ni kijana mwenye msimamao na anajua kutetea watu wake," Ruto alisema.

Naibu rais alikuwa akizungumza katika ziara ya kaunti ya Nyeri ambayo ni ya kwanza baada ya kumteua Gachagua kama naibu wake.

Wamumbu atawania ubunge wa Mathira kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi wa Agosti 9.

Ni yeye pekee aliyewasilisha ombi la kugombea kiti kwa tikiti ya UDA.

"Tulipokea ombi moja tu," chanzo ambacho hakiruhusiwi kuzungumza na wanahabari kilisema.

Juma UDA ilitoa wito wa wagombeaji waliotaka tikiti ya chama hicho kutuma maombi yao kabla ya Alhamisi, Mei 19.

Ruto alimteua Gachagua kama mgombea mwenza wake Jumamosi, Mei 15. Kabla ya kuteuliwa kwake Gachagua ndiye aliyeshikilia tikiti ya UDA katika eneo bunge la Mathira.