UDA yamteua mtu wa kwanza wa jinsia mbili kugombea kiti cha kisiasa

Muhtasari

• Kwamboka Kibagendi ambaye anajitambulisha kama mtu wa jinsia mbili atawania kiti cha MCA wa Mukuru Kwa Njenga katika uchaguzi wa Agosti.

•Kwa kuteuliwa kwa Kibagendi, wengi wanatumai kuwa watu zaidi na zaidi wa jinsia tofauti nchini Kenya watapata kutambuliwa na kulindwa zaidi kwa haki zao za kibinadamu.

Kwamboka Kibagendi apokea cheti cha uteuzi kuwania kiti cha Mukuru Kwa Reuben.
Kwamboka Kibagendi apokea cheti cha uteuzi kuwania kiti cha Mukuru Kwa Reuben.
Image: TWITTER// JINSIANGU

Chama kinachoongozwa na DP William Ruto kimemteua mtu wa jinsia mbili kuwania wadhifa wa umma katika kile ambacho kimetajwa kuwa kisa cha kwanza katika historia ya Kenya.

 Kwamboka Kibagendi ambaye anajitambulisha kama mtu wa jinsia mbili atawania kiti cha MCA wa Mukuru Kwa Njenga katika uchaguzi wa Agosti.

 Kibagendi atapeperusha bendera ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi wa Agosti 9.

 Shirika linalotetea haki za watu wenye jinsia mbili la Jinsiangu na watu wasiojitambulisha na jinsia yeyote nchini Kenya lilimpongeza Kibagendi kwa mafanikio hayo.

"Kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi wa Kenya, tuna mtu wa jinsia mbili anayegombea wadhifa.  Tunamtakia mafanikio katika azma yake ya kisiasa,” walisema.

Kwa muda mrefu sasa, watu wa jinsia mbili au watu waliozaliwa na sifa za kibayolojia za kiume na wa kike, wamekuwa wakipigania kutambuliwa kama jinsia ya tatu.

 Katika sensa ya 2019, hatua ndogo lakini muhimu ilichukuliwa baada ya kujumuishwa kwenye sensa. Kwa jumla walikuwa 1,524.

 Hofu ya unyanyapaa imewafanya wengi kuishi mafichoni, huku wengine wakikosa stakabadhi rasmi jambo linalofanya iwe vigumu kwao kuajiriwa.

Kwa kuteuliwa kwa Kibagendi, wengi wanatumai kuwa watu zaidi na zaidi wa jinsia tofauti nchini Kenya watapata kutambuliwa na kulindwa zaidi kwa haki zao za kibinadamu.

 Tayari, Bunge liliidhinisha uteuzi wa mtu wa kwanza wa jinsia tofauti kuchukua nafasi ya juu ya ofisi ya umma mnamo Februari. Dkt Dennis Nyongesa Wamalwa aliidhinishwa kushika wadhifa wa juu katika Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya.

(Utafsiri: Samuel Maina)