Didmus Barasa aandikisha taarifa baada ya kudaiwa kuweka rangi za UDA kwenye gari la serikali

Muhtasari

•Barasa aliandikisha taarifa baada ya polisi kuanzisha msako dhidi yake kwa madai kuwa alibadilisha rangi na nambari ya usajili ya gari la serikali kwa minajili ya kampeni zake.

•Bosi wa polisi katika kaunti ndogo ya Kimilili Mwita Maroa alisema kuwa gari hilo lenye nambari halisi ya usajili GK948J lilipatikana katika boma la mbunge huyo 

Gari linalodaiwa kubadilishwa rangina Barasa katika kituo cha polisi cha Bungoma
Gari linalodaiwa kubadilishwa rangina Barasa katika kituo cha polisi cha Bungoma
Image: JOHN NALIANYA

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amesema kuwa madai kuwa anatumia gari la serikali kufanya kampeni zake ni fitina za kisiasa.

Barasa aliandikisha taarifa Jumanne jioni baada ya polisi kuanzisha msako wa kumtafuta kwa madai kuwa alibadilisha rangi na nambari ya usajili ya gari la serikali kwa minajili ya kampeni zake.

Barasa amemlaumu mpinzani wake katika eneo la Kiminini kwa masaibu yake huku akimshtumu kwa kutumia njia za udanganyifu kuendeleza kampeni zake.

Tukutane kwa ground. Nimeandika taarifa yangu kwa polisi na kuwataka wasijiunge na timu yako ya kampeni,”Barasa alisema kupitia Facebook.

Jumanne Polisi na wenzao wa DCI katika kaunti ya Bungoma walianzisha msako wa kumtafuta Barasa kwa madai kuwa aliweka rangi na nembo ya UDA kwenye gari moja la eneo bunge lake.

Picha yake na ya Naibu Rais William Ruto pia zilibandikwa kwenye gari hilo.

Afisa mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Kimilili Mwita Maroa alisema kuwa gari hilo lenye nambari halisi ya usajili GK948J lilipatikana katika boma la mbunge huyo kijijini cha Nasianda Jumanne asubuhi.

"Tulifanya hivi katika oparesheni ya pamoja iliyohusisha maafisa wa kitengo cha ukaguzi wa serikali kutoka Nairobi, wafanyikazi wa uhalifu mkubwa, maafisa wa DCI kutoka Nairobi na Kimilili. Kikosi hicho kilivamia boma hilo kufuatia uchunguzi wa kina na kulivuta gari hilo hadi kituo cha polisi cha Kimilili na baadaye Bungoma kabla ya kuelekea. hadi Nairobi,” alisema.

Alisema polisi walipokea taarifa kutoka kwa wananchi waliotoa malalamiko yao baada ya kuliona gari hilo katika mikutano ya kampeni za mbunge huyo.

Marua alisema kuwa gari hilo lilikuwa na nambari ghushi ya KBS 709D.

Alisema kuwa ni kinyume cha sheria kutumia magari ya serikali kwa masuala ya kibinafsi na masuala ya kampeni.

Marua alisema kuwa mbunge huyo ambaye alidaiwa kuenda mafichoni alikuwa anatafutwa kujibu mashtaka ya kughushi, na wizi wa gari la serikali miongoni mwa makosa mengine makubwa.

Polisi walisema kwa taarifa za awali, namba za usajili zilizokuwa zimeghushiwa ni za ndugu wa mbunge huyo.

Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai kaunti ya Bungoma alisema kuwa wapelelezi wamewasiliana na NTSA jijini Nairobi ili kuthibitisha ikiwa gari hilo limesajiliwa chini yao.