Ruto anaongoza umaarufu kwa pengo ndogo dhidi ya Raila- Kura ya Maoni

Muhtasari

•Kura ya maoni ya hivi punde ya Radio Africa inaonyesha kuwa Ruto amejizolea asilimia 43.3 dhidi ya asilimia 42.4 ya Raila .

•Ruto angali anaongoza  katika Jimbo la Kati kwa uungwaji mkono wa asilimia 52 ikilinganishwa na asilimia 32.2  za Raila. 

Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga
Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga
Image: STAR

Uchaguzi wa urais mnamo Agosti 9 umekuwa mbio za farasi wawili huku  naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga wakipelekana hapa kwa hapa.

Kura ya maoni ya hivi punde ya Radio Africa inaonyesha kuwa Ruto amejizolea asilimia 43.3 dhidi ya asilimia 42.4 ya Raila  kutokana na majibu ya waliohojiwa kuhusu nani wanapendelea kuwa rais wao.

Lakini kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ana uungwaji mkono wa asilimia 4.0 unaomruhusu kuwa mhusika na kuwazuia Raila na Ruto kupata ushindi wa raundi ya kwanza.

Mwangi wa Iria pekee ndiye anayejitokeza vile vile akiwa na asilimia 2.3 huku Wengine ni asilimia 1.9 na Asilimia 6.1 bado hawajafanya maamuzi.

Utafiti wa Redio Afrika unaotegemea mahojiano ya  ujumbe mfupi na waliohojiwa  ni wapiga kura 3,559 katika kaunti zote 47. Utafiti una asilimia 4.5 ya makosa, jambo ambalo linafanya kuwa vigumu kubainisha kiongozi halisi.

Hata hivyo ikilinganishwa na mwaka jana, uungwaji mkono wa Raila kama rais umepanda kwa kasi kutoka asilimia 20.0 katika tafiti za Radio Afrika hadi zaidi ya asilimia 42 hivi leo huku uungwaji mkono wa Ruto ukiongezeka kidogo kutoka asilimia 39 hadi 43.

Katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho kimepita, serikali imekuwa ikiegemea upande wa Raila huku Rais Uhuru Kenyatta akiweka wazi zaidi kumuunga mkono Raila na kumpinga Naibu Rais Ruto.

Katika uchaguzi wa 2013, ushirikiano kati ya Ruto na Uhuru uliegemezwa kwenye ahadi ya wazi kwamba Uhuru angehudumu mihula miwili kama Rais na kufuatiwa na mihula miwili ya Ruto kama Rais.

Ruto angali anaongoza  katika Jimbo la Kati kwa uungwaji mkono wa asilimia 52 ikilinganishwa na asilimia 32.2  za Raila. Hata hivyo  pengo kati yao limepungua kutoka asilimia 40 hadi 20 katika muda wa miezi sita iliyopita.

Ruto pia anaongoza katika eneo la Bonde la Ufa Kaskazini kwa asilimia 68.9 ikilinganishwa na 22.6 za Raila, Kusini mwa Rift kwa asilimia 51.5 ikilinganishwa na Raila 35.1 , na Mashariki ya Juu kwa asilimia 58.6 dhidi ya 27.8 zake Raila.

Kwingineko Raila anaongoza ingawa mara nyingi mbio huwa karibu sana. Pwani, Raila ana asilimia 49.7 dhidi ya asilimia 39.1 ya Ruto; katika Mashariki ya Chini, Raila ana asilimia 37.4 dhidi ya 35.2 za Ruto.

Jijini Nairobi, Raila ana asilimia 53.4 dhidi ya 34.3 ya Ruto; Kaskazini Mashariki, Raila ana asilimia 46.6 dhidi ya 40.4 za Ruto; katika eneo la Magharibi Raila anaongoza kwa asilimia 44.8 huku Ruto akiwa na 38.8; na huko Nyanza anaongoza kwa asilimia 69.6 dhidi ya asilimia 17.17 ya Ruto.

Bado kuna mienendo mikubwa katika upendeleo wa wapigakura kwa hivyo wiki nne zijazo zitakuwa muhimu.

Katika eneo la Magharibi, muungano wa Musalia-Wetang'ula unaonekana kukiuka msingi wa kijadi wa Raila. Ruto ameunganisha Bonde la Ufa Kusini huku Raila akipata Mashariki ya Chini na Kaskazini Mashariki, maeneo yote mawili yenye ushindani mkali. Raila pia ameunganisha Nairobi.

Wakati huo huo Kalonzo ana uungwaji mkono mkubwa wa asilimia 17.1 katika Mashariki ya Chini.

Umuhimu wa mbio hizo unasisitizwa sio tu na asilimia 6.1 wanaosema hawajaamua bali pia na asilimia 28.0 wanaosema kuwa hawawezi kupiga kura, ambapo asilimia 5.1 wanasema 'pengine' hawatapiga kura na asilimia 5.8 kwamba 'hawatapiga kura.

Iwapo wananchi hao wangehamasishwa kupiga kura, ingetosha kushinda uchaguzi wa Raila au Ruto. 

Suala kubwa linalowakabili wapiga kura ni gharama ya juu ya maisha, kulingana na asilimia 62.3 ya washiriki ikifuatiwa na ukosefu wa ajira (asilimia 16.3); rushwa 11.0; umaskini 2.7; uhaba wa chakula 2.1; huduma duni za afya 2.0 na wengine asilimia 3.5.

(Utafsiri: Samuel Maina)