Tutapata nafasi 6 katika Baraza la Mawaziri- Wetangula awaambia Waluhya

Muhtasari
  • Ford Kenya na ANC vitapata nafasi sita za Baraza la Mawaziri ikiwa muungano wa Kenya Kwanza utashinda uchaguzi wa urais
  • Wetangula  alitoa wito kwa jamii ya Mulembe kupigia kura Kenya Kwanza akisema hapo ndipo maslahi yao yatazingatiwa
Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula kwenye mkutano wa kisiasa katika wadi ya Soysambu eneo bunge la Tongaren.
Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula kwenye mkutano wa kisiasa katika wadi ya Soysambu eneo bunge la Tongaren.
Image: JOHN NALIANYA

Vyama vya Ford Kenya na ANC vitapata nafasi sita za Baraza la Mawaziri ikiwa muungano wa Kenya Kwanza utashinda uchaguzi wa urais, Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula amesema.

Akizungumza  Jumatano katika wadi ya Soysambu, eneo bunge la Tongaren, Wetang'ula alisema hayo ndiyo makubaliano waliyoweka kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa na IEBC. 

"Ford Kenya na ANC zikiwa wanachama waanzilishi wa miungano ya Kenya Kwanza zitakuwa na asilimia 30 ya Baraza la Mawaziri na uteuzi mwingine wowote," Wetang'ula alisema.

Aidha alisema asilimia 30 inatumika hata katika uteuzi mwingine, wakiwemo makatibu wakuu na nafasi za mabalozi.

 Seneta huyo alitoa wito kwa jamii ya Mulembe kupigia kura Kenya Kwanza akisema hapo ndipo maslahi yao yatazingatiwa. 

Alisema ameridhishwa na kuwa seneta wa Bungoma na nyadhifa anazopigania ni za jamii na sio yeye mwenyewe. Wetang'ula alisisitiza kuwa yeye si mbinafsi na atahakikisha kwamba biashara zake zote zinalenga kuwezesha jamii. 

Alihakikishia jamii ya Waluhya kwamba makubaliano waliyofanya na Ruto yataheshimiwa huku akidai kuwa naibu rais ana historia ya kutimiza ahadi zake.

 “Tofauti na Raila Odinga, Ruto hana historia ya usaliti na ninawahakikishia watu wetu kwamba kama wakili tuna mpango mzuri naye,” akasema. 

Pia alisema kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na yeye mwenyewe ndio viongozi wakuu wa eneo la Magharibi na kwamba mgombea urais bila baraka zao hatapata kura. 

"Sisi ndio safu ya kwanza na ya mwisho ya utetezi wako kwa hivyo sikiliza mwelekeo wetu na upigie kura Kenya Kwanza," seneta huyo alisema.

"Kwa muda mrefu mgawanyiko katika jamii ya Waluhya umekuwa kwa sababu ya Maragolis na Bukusus, lakini kwa muungano wetu, mchezo umekwisha." 

Musalia aliwaambia wale wanaounga mkono Azimio katika eneo la Magharibi kukoma kukosoa makubaliano yao ya 30%  lakini badala yake wawaambie wakazi kile ambacho wameafikiana kwa upande mwingine. 

Alisema makubaliano ya awali ya uchaguzi wa Azimio hayakuwa wazi na ndiyo maana Magavana Alfred Mutua na Amason Kingi walijiondoa.