Mwangi wa Iria aongoza maandamano Bomas kupinga hatua ya IEBC kuondoa jina lake kwa sajili wa wagombea

Muhtasari

• Siku ya Jumapili usiku, gavana huyo wa Murang'a alizua taharuki baada ya kupata jina lake halipo kwenye sajili, licha ya kuwasilisha mahitaji yote ya awali. 

• Wa Iria ambaye aliandamana na wafuasi wake aliziba lango la Bomas akilalamikia kuondolewa kwa jina lake kutoka sajili ya IEBC ya wagombeaji wa urais kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mgombea urais wa chama cha Usawa Kwa Wote Mwangi wa Iria akiandamana katika ukumbi wa Bomas of Kenya baada ya jina lake kufutwa kwenye ratiba ya IEBC ya uteuzi wa urais mnamo Mei 30, 2022. Picha: EZEKIEL AMING'A
Mgombea urais wa chama cha Usawa Kwa Wote Mwangi wa Iria akiandamana katika ukumbi wa Bomas of Kenya baada ya jina lake kufutwa kwenye ratiba ya IEBC ya uteuzi wa urais mnamo Mei 30, 2022. Picha: EZEKIEL AMING'A

Mgombea urais wa chama cha Usawa Kwa Wote Mwangi Wa Iria siku ya Jumatatu aliziba lango la Bomas of Kenya. 

Wa Iria ambaye aliandamana na wafuasi wake aliziba lango la Bomas akilalamikia kuondolewa kwa jina lake kutoka sajili ya IEBC ya wagombeaji wa urais kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9. 

Alisema mtu anayeitwa Sunkuli, ambaye alidai kuwa ni afisa wa IEBC, alimweleza kuwa jina lake liliondolewa kwenye orodha hiyo kwa sababu "Mawazo yangu binafsi ni kwamba tunapoleta saini hapa baadhi ya watu wanaziuza kwa sababu hakuna vile unaweza kukubali hati zangu, hunipi majibu halafu siku saba baadaye ninapouliza, unanitumia watu kwa njia isiyo rasmi," Wa Iria alisema. 

Maafisa wa usalama wakishika doria katika ukumbi wa Bomas of Kenya baada ya mgombea urais wa chama cha Usawa Mwangi Wa Iria na wafuasi wake kuandamana kupinga kuondolewa kwa jina lake. Picha: EZEKIEL AMING'A
Maafisa wa usalama wakishika doria katika ukumbi wa Bomas of Kenya baada ya mgombea urais wa chama cha Usawa Mwangi Wa Iria na wafuasi wake kuandamana kupinga kuondolewa kwa jina lake. Picha: EZEKIEL AMING'A

Aliishutumu tume hiyo kwa kutumia njia zisizo rasmi kuwasiliana naye na wamekuwa wakimkwepa. Kuna maafisa wengi wa polisi katika ukumbi wa Bomas of Kenya huku wafuasi wake wakiimba nyimbo za "No Wa Iria, no election". 

Siku ya Jumapili usiku, gavana huyo wa Murang'a alizua taharuki baada ya kupata jina lake halipo kwenye sajili, licha ya kuwasilisha mahitaji yote ya awali. 

"Hata watu ambao walishindwa kukidhi mahitaji yenu wako kwenye ratiba lakini jina langu limeondolewa... Hakuna uchaguzi utakaofanyika ikiwa sitagombea," alisema. 

Picha: EZEKIEL AMING'A
Picha: EZEKIEL AMING'A

Wa Iria alisisitiza kuwa aliafiki mahitaji yote, ikiwa ni pamoja na kuleta saini kutoka kwa wafuasi katika kaunti 24 inavyohitajika na tume hata ikakubali kupokelewa. 

"Hatuwezi kuanza kuiba sasa ... Wameondoa jina langu kwa makusudi leo." 

Mwaniaji huyo wa urais wa Usawa Kwa Wote alitoa wito kwa wafuasi wake wote kuandamana naye kwenye mkutano na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati siku ya Jumatatu.