Reuben Kigame afungiwa nje ya kivumbi cha urais 2022

Muhtasari

• Mgombea urais Reuben Kigame amefungiwa nje ya kinyang'anyiro hicho na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). 

Mgombea urais Reuben Kigame akihutubia wanahabari nje ya jumba la Anniversary Tower Nairobi, baada ya jaribio lake kukutana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kugonga mwamba./WILFRED NYANGARESI
Mgombea urais Reuben Kigame akihutubia wanahabari nje ya jumba la Anniversary Tower Nairobi, baada ya jaribio lake kukutana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kugonga mwamba./WILFRED NYANGARESI

Mgombea urais Reuben Kigame amefungiwa nje ya kinyang'anyiro hicho na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). 

Kigame ambaye aliwasilisha stakabadhi zake kwa IEBC ili kuidhinishwa alithibitisha Jumatatu kwenye kikao cha wanahabari kwamba amezuiliwa kushiriki kinyang'anyiro cha urais cha mwaka 2022.

 Alisema aliambiwa na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Jumapili saa nne usiku kwamba alikosa kutimiza masharti ya kufuzu kuania urais. 

Jaribio la Kigame kukutana na mwenyekiti wa IEBC siku ya Jumatatu liliambulia patupu kwani hakupewa hadhira.

 "Nilipotaka kutafuta hadhira kwa Mwenyekiti na kupata suluhu kwa suala hili, walinzi walinizuia kuingia Bomas of Kenya wakisema hakuna mgombea anayeruhusiwa," alisema. 

Mwingine anayekabiliwa na changamoto sawia na Kigame ni Gavana wa Murang'a Mwani Wa Iria ambaye alipinga jina lake kutojumuishwa katika orodha ya wawaniaji urais iliyoratibiwa kuidhinishwa.